Zenj FM

Jamii yahimizwa kufanya usafi ili kuepukana na maradhi ya matumbo

30 May 2024, 6:10 pm

Wanafunzi wa ZU wakifanya usafi katika eneo la Unguja Ukuu.

Na Mary Julius.

Jamii imetakiwa kuendelea kudumisha suala la usafi katika maeneo yao ili kuweza kujikinga na maradhi mbali mbali pamoja na kuifanya Miji kuwa nadhifu.

Hayo yameelezwa na viongozi wa afya pamoja na Wanafunzi wa ZU (Zanzibar University) wakati walipokuwa wakifanya usafi katika maeneo ya Unguja Ukuu.

Akizungumza na wanafunzi hao Afisa Mazingira wa Baraza la Mji Kati Is-haq Kombo  Abdallah amesema usafi huu hufanyika kila ifikapo tarehe 22 ya kila mwezi lengo ikiwa ni kujilinda na kujiepusha na maradhi nyemelezi hasa katika kipindi hichi ambacho maradhi hayo yameenea kwa wingi.

Aidha amesisitiza kuwa jukumu la usafi ni la kila mmoja wetu na ndio maana wameamua kuufanya usafi huo pamoja na wanafunzi hao ili kuwakumbusha kuwa usafi ni muhimu katika mazingira yoyote yaliyomzunguka mwanadam na ni wajibu wa kila mmoja.

Sauti ya Afisa Mazingira wa Baraza la Mji Kati Is-haq Kombo  Abdallah.

Nae afisa wa afya Ame Suleiman Abdallah ambae ni mwanafunzi kutoka chuo kikuu cha Zanzbar University ametoa wito kwa wanafunzi wenzake pamoja na wananchi kuendelea kushirikiana na maafisa wa afya kutoka Baraza la Mji Kati katika kufanya usafi katika maeneo yanayo wazunguka ili kuweza kujiepusha na maradhi.