Mbeto amjibu Jussa kuhusu uingizaji wa mafuta Zanzibar
27 May 2024, 4:52 pm
Na Mary Julius
Makampuni ya ndani uwezo wao wa mitaji umeyumba kutokana na bei ya mafuta kupanda duniani inayosababishwa na uwepo wa vita vya Urusi na Ukraine.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis, amewataka viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo kuacha upotoshaji juu ya mchakato wa zabuni za kampuni za uingizaji wa mafuta nchini kwani kampuni ya GBP ndiyo iliyokidhi vigezo na kupewa tenda hiyo kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na Zenji Fm Katibu Khamis ametoa ufafanuzi juu ya hoja zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar Ismail Jussa wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa chama hicho mkoa wa Kusini Unguja, aliyedai kuwa kuna mikataba mingi mibovu inayogharimu nchi.
Amesema mchakato huo ulikuwa wazi kwa kampuni yoyote iliyokuwa na uwezo wa kuingiza mafuta itimize masharti mbalimbali yakiwemo kutoa huduma hiyo kwa wakati wote pia kulipwa fedha kidogo kidogo na wakati mwingine kwa mkopo vigezo ambavyo makampuni zaidi ya matano yalikataa kwa kudai kuwa yanahitaji kulipwa fedha taslimu kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani, vigezo ambavyo kampuni GBP ilikubali kutekeleza.
Mbeto, amesema Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, imeendelea kufanya juhudi kubwa za kuhakikisha inafunga mikataba halali na yenye maslahi mapana ya nchi.
Aidha Katibu huyo wa NEC Mbeto, amesema makampuni yanayolalamika kutopewa tenda hiyo mengi hayana mtaji wa kutosha katika kuleta mafuta ya kukidhi soko la Zanzibar, hivyo wasitumie baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaofanya siasa za kiharakati kupandikiza mbegu za chuki kwa wananchi na kuharibu hadhi ya nchi katika soko la kikanda na kimataifa.