Maji safi na salama tatizo sugu Kiungani
8 April 2024, 5:00 pm
Ongezeko la watu, kukatika kwa umeme mara kwa mara katika shehia ya Kiungani kumesababisha ukosefu wa maji safi na salama katika shehia hiyo.
Na Rahma Hassn na Suleima Abdalla
Wakazi wa Nungwi shehia ya Kiungani mkoa wa Kaskazini Unguja wameiomba Mamlaka ya Maji Zanzibar ZAWA kuwafikishia huduma ya maji safi na salama katika shehia hiyo ambayo zaidi ya miezi mitatu haijapata huduma hiyo.
Wakizungumza na Zenji Fm wamesema kukosekana kwa maji katika shehia hiyo kunapelekea kutembea umbali mrefu ili kufuata huduma hiyo hali ambayo inahatarisha maisha ya wanawake na watoto wa shehia hiyo.
Aidha wakazi hao wamewaomba wawekezaji hasa wa mahotel kuwasogezea huduma hiyo ambayo inapatikana katika maeneo yao.
Naye sheha wa kiungani Makame Machu Ali amekiri kuwepo kwa changamoto ya maji katika shehia yake.
Diwani wa wadi ya Bandakuu Siti Ali Makame amesema asili ya maeneo ya Nungwi yana shida ya upatikanaji wa maji safi hali iliyopelekea kuchimba visima katika maeneo ya jirani.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mamlaka ya Maji Zanzibar Zawa Abeid Mussa Suleiman amesema mamlaka imechukua hatua ya ufumbuzi wa changamoto hiyo katika shehia ya kiungani kwa kufunga mkataba na mradi wa NEC kutoka nchini Oman ambo umegharimu dola milioni 26 wa ajili ya kuhakikisha shehia hiyo inapata maji safi na salama.