Taasisi za kiraia,Pemba zamwaga neema kwa wananchi
19 March 2024, 4:30 pm
Na Is-haka Mohammed.
Meya wa Manispaa ya Chake Chake Abdalla Hamad Abdalla amesema kazi za utoaji wa misaada na sadaka zinazofanywa na taasisi mbali mbali za kiraia zinaisaidia serikali kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Meya ameyasema hayo katika hafla ya kukabidhi sadaka kwa ajili ya futari kwa wananchi wasiojiweza na wenye uhitaji zilizotolewa na Taasisi ya Tawakal Foundation Iftar kwa kushirikiana na Taasisi ya Takrima huko Vitongoji Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema serikali imekuwa ikifarijika kuona taasisi hizo zimekuwa zikiisaidia kutatua changamoto mbali za wananchi.
Kwa upande wake Katibu wa Taasisi ya Tawakal Faundation Salma Abdalla Hemed ameomba taasisi kuendelea kutoa sadaka zao za Ramadhani kwani kuna uhitaji katika maeneo mbali mbali.
Nao baadhi ya wananchi waliopatiwa sadaka hizo wametoa shukrani zao kwa taasisi hiyo na kuwaombea dua wale waliochanga sadaka hizo hadi kuwafikia wao.
Miongoni mwa sadaka zilizotolewa na pamoja na Mchele, Sukari, Maharage, Tambi, Kanga, Mabaibui na Viatu ambapo jumla ya waislamu 85 wa kijiji hicho wamepatiwa sadaka hiyo.