Mabadiliko ya tabia ya nchi, kikwazo kwa mapambano dhidi ya malaria Zanzibar
18 March 2024, 5:07 pm
Na Mary Julius.
Zanzibar imepiga hatua kubwa ya kumaliza malaria licha ya kutokea mlipuko wa maradhi katika siku za hivi karibuni .
Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa na wadau wengine kuhakikisha kuwa maradhi ya malaria yanaondoka hapa nchini.
Akifungua mkutano wa siku moja wa Mpango Kazi kwa mwaka 2025 uliowashirikisha wadau na mashirika ya kimataifa, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Salim Slim amesema jitihada zinafanyika kwa wananchi juu ya kujikinga na maradhi hayo.
Amesema katika kipindi cha miaka kumi na saba mpaka ishirini nyuma, Zanzibar iliweza kufanya mambo makubwa ya kudhibiti maradhi ya malaria kwa kiasi kikubwa, hata hivyo katika kipindi cha hivi karibuni kulitokea mlipuko wa maradhi hayo yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema kutokana na hali hiyo Wizara ya Afya kwa kushirikana na mashirika ya kimataifa na wadau wengine waliweza kufanya kazi kubwa ya kudhibiti maradhi hayo ambapo kwa sasa maradhi hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini na kuwataka wananchi kutumia kinga dhidi ya maradhi hayo.
Kwa upande wa Meneja wa Programu ya kumaliza Malaria Zanzibar Shija Joseph Shija amesema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wanaosaidia mapambano dhidi ya malaria na kuandaa mpango kazi wa mwaka mmoja na kuwasilisha na kuweza kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya matumizi.
Aidha amewasisitiza wananchi kuendelea kukubali kazi zinazofanywa na programu ya kumaliza malaria kwa jamii na kuzingatia mbinu ya kujikinga na maradhi hayo ikiwemo kulala kwenye chandarua, upigaji dawa majumbani pamoja kuweka usafi wa mazingira.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa kupambana na maradhi ya Malaria, Kifua Kikuu na Ukimwi katika Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Dkt. Abdallah Suleiman amesema kazi kubwa wanayoifanya ni kusaidia katika kutafuta fedha, wataalam ili kuweza kuendeleza kazi kwa mujibu wa muda uliopangwa.