Wizara ya Afya Zanzibar yatoa ripoti vifo vya watoto tisa
12 March 2024, 6:45 pm
Na Mary Julius
Kufuatia vifo vya watoto tisa waliofariki kwa kula nyama ya kasa, Wizara ya Afya Zanzibar imewataka wananchi visiwani humo kuacha kula nyama hiyo.
Wizara ya Afya Zanzibar imetoa ripoti ya utafiti uliofanywa kufuatia watoto tisa kufariki dunia na wengine wakiendelea kupatiwa matibabu baada ya kusadikiwa kula nyama ya kasa ambayo imesababisha madhara makubwa.
Akitoa ufafanuzi wa ripoti hiyo, Naibu Waziri Wizara ya Afya Hassan Khamis Hafidh amesema tukio hilo limeripotiwa Machi 6 mwaka huu katika kijiji cha Kisiwa Panza mkoa wa Kusini Pemba na wengine takribani 160 wameathirika na nyama hiyo na kupatiwa matibabu,
Akitoa taarifa ya kitaalam mkemia mkuu wa serikali Faridi Mpatani amesema kufuatia uchunguzi wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali kwa kushirikiana na mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali ya Tanzania Bara, ripoti imebaini kuwepo kwa aina ya sumu iliyopatikana katika sampuli zote zilizokusanywa katika tukio hilo.
Naye Naibu Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Fatma Kabole amesema Wizara bado inaendelea kutoa elimu pamoja na kufuatilia wagonjwa ili kuhakikisha wahanga wa madhara hayo wanapatiwa matibabu