Jamii yatakiwa kuona umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari
11 March 2024, 5:12 pm
Na Mary Julius.
Mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahamoud amesema serikali inahitaji kuwa na akiba ya kutosha ya damu salama ili kuokoa maisha ya watu pale wanapokabiliwa na majanga.
Akizungumza katika zoezi la uchangiaji damu huko kiwanja cha Bungi Wilaya ya Kati Ayoub amesema hatua hiyo ni kuwahakikishia usalama wale wote wenye mahitaji ya damu salama hasa wanapopatwa na ajali na mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Aidha amesema serikali kupitia kitengo cha damu salama na taasisi nyengine itaendelea kuwahamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuwa na akiba ya kutosha ya damu salama hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Naye Mkugenzi matukio wa ZBC Salum Ramadhan Abdalla na Afisa uhusiano wa kitengo cha damu salama Ussi Bakari Mohamed Wamesema wameanzisha kampeni hiyo ya Mwavuli wa damu salama ili kusaidia makundi mbali mbali ya jamii na kupongeza ushiriki mkubwa wa wananchi katika zoezi hilo ambapo kampeni hiyo imelenga kupata chupa mia sita na hamsini kwa Mkoa huo.
Nao wananchi walioshiriki katika zoezi la uchangiaji damu Ramadhan Pandu Haji na ndugu Munira Mmanga Mohd wamesema ni vyema kwa jamii ikaona umuhimu wa suala la kuchangia damu kwa hiari ili kuwasaidia wagonjwa watakaokuwa na mahitaji nchini.