Radio Jamii Kilosa

DC Kilosa aagiza hatua dhidi ya wafugaji

16 October 2026, 14:08

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka akiwa katika mkutano wa hadhara kijiji cha Nyali. Picha na Stamius Kyombo

Jamii imetakiwa kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji ili kumaliza migogoro inayotokana na mifugo kuingia mashambani na kuharibu mazao ya wakulima, kwa kuzingatia sheria.

Na Asha Madohola

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, amefanya ziara katika Kijiji cha Madudumizi, Kata ya Zombo, wilayani Kilosa, kwa lengo la kujionea uharibifu wa mazao ya wakulima unaosababishwa na mifugo inayoingizwa katika mashamba yao. Katika ziara hiyo, ameambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.

Mwananchi wa kijiji cha Madudumizi Bi Habiba Segasega mmoja wa wakulima aliyelishiwa shamba la mahindi na ng’ombe

Akiwa kijijini hapo, Mhe. Shaka amezungumza na wakulima walioathirika, ambao wameeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya wafugaji kuruhusu mifugo yao kuingia mashambani na kula mazao pia walisema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwasababisha kutumia muda mwingi kukaa mashambani wakilinda mazao yao dhidi ya uharibifu unaofanywa na mifugo hiyo.

Aidha wakulima hao walimpongeza Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi alioambatana nao kwa kufika eneo hilo kujionea changamoto wanayokabiliana nayo, wakieleza matumaini yao kuwa hatua zitakazochukuliwa zitasaidia kulinda mazao yao na kuimarisha uhusiano kati ya wakulima na wafugaji.

Sauti ya mkulima Bi Habiba Segasega akizungumza
Shamba la maharage lililoharibiwa na ng’ombe katika kijiji cha Madudumizi

Baada ya kujionea uharibifu huo, Mhe. Shaka ameelekeza kufanyika kwa tathmini ya mazao yaliyoharibiwa ili kubaini kiwango cha hasara iliyopatikana na kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa mifugo watakaobainika kuhusika. Hatua hiyo inalenga kulinda haki za wakulima na kuhakikisha sheria na taratibu zinazohusu ufugaji na kilimo zinafuatwa.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka akizungumza
Wananchi wa kijiji cha Nyali wakiwa katika mkutano wa hadhara na Mkuu wa wilaya ya Kilosa