Radio Jamii Kilosa

Ukatili hauna nafasi kwa vijana Kilosa

21 July 2026, 16:11

Wanafunzi wa chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa wakifuatilia mafunzo ya jinsia ambayo yalitolewa na Smaujata. Picha na Asha Madohola

Ukatili ni kitendo chochote kinachosababisha maumivu, madhara au mateso kwa mtu mwingine, iwe ni kimwili, kingono, kisaikolojia, kihisia au kiuchumi na unaweza kutokea nyumbani, shuleni, kazini au katika jamii hivyo ni muhimu kutoa taarifa mapema

Na Asha Madohola

Vijana nchini wametakiwa kuvunja ukimya kwa kutoa taarifa mara wanapoona au kufanyiwa vitendo vya ukatili ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wakati na wahusika kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria. Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Morogoro, Joyce Nyangi, wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Maafisa Tabibu wilayani Kilosa kuhusu namna ya kutambua, kujikinga na kuripoti vitendo vya ukatili.

Mwenyekiti wa Smaujata mkoa wa Morogoro Joyce Nyangi akizungumza mara baada ya mafunzo

Akizungumza katika mafunzo hayo, Nyangi alieleza kuwa vijana wanapaswa kufahamu aina mbalimbali za ukatili ikiwemo ukatili wa kimwili, kingono, kisaikolojia na kiuchumi ili waweze kujilinda na kuwasaidia wengine wanaokumbana na changamoto hizo. Aidha, aliwahimiza kutumia namba ya huduma ya watoto 116 kutoa taarifa za ukatili kwa haraka ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua stahiki.

Sauti ya Mwenyekiti wa Smaujata mkoa wa Morogoro Joyce Nyangi akizungumza
Dkt Diana ambaye ni Mkufunzi chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa

Kwa upande wake, mkufunzi wa Chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa, Dkt. Diana, alisema kabla ya mafunzo hayo wanafunzi wengi walikuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya ukatili na namna ya kuyashughulikia. Alimshukuru mtoa mafunzo kwa elimu hiyo muhimu na kuwataka wanafunzi kujitambua, kuwa waangalifu katika kipindi hiki cha utandawazi na kufanya maamuzi sahihi yatakayowalinda dhidi ya vitendo vya ukatili.

Dkt Diana ambaye ni Mkufunzi chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa akizungumza
Mwanafunzi Shabani Ramadhan Mahamudu

Nao baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Shaban Mahamudu na Charity Mloge, walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata wakisema imewajengea ujasiri wa kutambua na kuripoti vitendo vya ukatili na waliahidi kuifikisha elimu hiyo kwa vijana wengine katika jamii ili kuongeza uelewa na kuhamasisha vijana kutokuwa waoga wa kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili.

Sauti za wanafunzi wakizungumza
Picha ya pamoja ya viongozi Smaujata, mkufunzi na wanachuo