Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
1 August 2026, 10:45

Wiki ya Unyonyeshaji Duniani huadhimishwa kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi 7, ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama katika kuhakikisha watoto wanapata afya bora, lishe sahihi na ukuaji unaofaa.
Na Asha Madohola
Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imezindua maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani katika Zahanati ya Rudewa, Kata ya Rudewa, kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa maziwa ya mama na unyonyeshaji sahihi wa watoto.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Elisha Kingu, amesema jamii imepewa elimu kuhusu namna sahihi ya kumnyonyesha mtoto, kumshika wakati wa kunyonyesha na kutambua iwapo mtoto anapata maziwa ya kutosha na alisema elimu hiyo itaendelea kutolewa kuanzia Agosti 1 hadi 7, 2026, kupitia vituo vya afya na vyombo vya habari, kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo na kupunguza changamoto za utapiamlo.

Kwa upande wake, Afisa Tarafa wa Kimamba, Sabina Lucas Sugwa, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, amewataka akina mama kutimiza wajibu wa kuwanyonyesha watoto wao na kuwataka wataalamu wa afya pamoja na viongozi kuendelea kutoa elimu na hamasa kuhusu unyonyeshaji na malezi bora ya watoto.
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Rudewa, David Philemon Mkuchu aliushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa pamoja na wadau kwa kuichagua zahanati hiyo kuwa mwenyeji wa uzinduzi huo, akisema tukio hilo limekuwa chachu kwa watumishi wa afya na wananchi wa Rudewa katika kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji.

Akizungumza kwa niaba ya akina mama walioshiriki uzinduzi huo, Raheli Lazaro kutoka Rudewa, alisema amefurahishwa na elimu aliyopata, ikiwemo namna sahihi ya kumnyonyesha mtoto, lishe inayofaa kwa mama anayenyonyesha na umuhimu wa mtoto kupata maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo pia elimu hiyo imewasaidia kufahamu umuhimu wa wazazi kushirikiana katika malezi na kuhakikisha watoto wanapata uangalizi, upendo na malezi bora tangu wakiwa wadogo.
