Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
16 August 2026, 10:24

Uzalendo na kutii sheria za nchi ni msingi wa kujenga jamii yenye amani, usalama na maendeleo ambapo pia husaidia kuzuia uhalifu, migogoro na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Na Asha Madohola
Mkuu wa Kituo cha Polisi Kilosa, Afande Donati Mhina, alishiriki mazishi ya Askari Mgambo MG Ally Ramadhani, ambaye pia alikuwa mdau wa kituo cha Redio Jamii Kilosa maarufu kama Kanda Bovu, yaliyofanyika katika Kata ya Kidete, Wilaya ya Kilosa, na kuzikwa katika makaburi ya eneo hilo.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Afande Mhina alimtaja marehemu kuwa miongoni mwa askari wazalendo na anayekubalika sana katika jamii, huku akieleza kuwa mchango wake katika kulinda usalama na kushirikiana na jamii utaendelea kukumbukwa.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na kuepuka vitendo vya uhalifu na kuzingatia sheria, akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kuwa sehemu ya juhudi za kulinda amani na usalama katika jamii.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na zaidi ya wananchi 1,500 kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kilosa, ambao walifika Kidete kumuaga kwa mara ya mwisho Askari Mgambo MG Ally Ramadhani, maarufu kama Kanda Bovu na Redio Jamii Kilosa itamkumbuka kwa machango wake alioutoa enzi ya uhai wake katika ushiriki wake wa kutoa maoni katika vipindi mbalimbali.
