Radio Jamii Kilosa

Bilioni 7.9 kukamilisha ujenzi wa daraja Berega

6 July 2023, 7:35 am

Ujenzi wa daraja la Berega ukiendelea. Picha na Gladys Mapeka

Kukamilika kwa daraja la Berega kutawaondolea adha ya muda mrefu ya upatikanaji wa usafiri waliyokuwa wanakabiliana nayo wananchi wa kata ya Berega ambayo ilichangia wananchi kupoteza maisha wakivuka kwenye mto wakati wa masika ili kufuata mahitaji muhimu ya kijamii.

Viongozi wa eneo hili wanatakiwa kuhakikisha wanalisimamia na kulilinda daraja hili kwa kutoa elimu kwa wananchi kuepuka kufanya shughuli zozote za kibinadamu pembezoni mwa mto kufanya shughuli zozote ambazo zitasababisha mmomonyoko wa ardhi.

Na Asha Madohola

Mhe Denis Londo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu Bunge ya Tamisemi

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Denis Londo ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa kijiji cha Berega kata ya Berege kulitunza na kulilinda daraja ya Berega –Dumbalume linalojengwa chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na mijini (TARURA).

Mhe Londo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi unaoendelea katika daraja hilo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro aliambatana na wajumbe wa Kamati hiyo.

“Fedha zilizotumika kujenga daraja hili ni dhahiri kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuwaondoa wananchi wake katika umasikini kwani uwepo wa miundombinu bora ya barabara inarahisisha huduma za kijamii kama Hospitali na usafiri” alisema Mhe Londo

Mhandisi Mkazi Bw David Mwakalalile

Awali akisoma Taarifa ya mradi Mhandisi Mkazi Bw. David Mwakalalile alisema daraja hilo lina urefu wa mita 140 na upana wa mita 11 linalojengwa chini ya Mkandarasi Nyaza Road Works Limited Mwanza litagharimu shilingi Bilioni 7.9 na atasimamia mradi huo kwa ubora na ukamilike kwa wakati.

Prof Palamagamba Kabudi akizungumza

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi alishukuru Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwa wananchi sio tu kwa usafirishaji wa biashara zao lakini pia kutatua changamoto zilizokuwa zinatokea kwani wapo watu waliopoteza maisha kabla ya kuwepo kwa daraja hilo.