Radio Jamii Kilosa

Mapato ya Halmashauri ya Kilosa yaongezeka na kufikia asilimia 98.9

9 September 2023, 2:19 pm

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba. Picha na Elizabeth Makemba

Katika kipindi cha miaka miwili Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujenga shule za Awali, Msingi na Sekondari mpya ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi.

“Tumefanikiwa kuwafikia wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufika shuleni katika miradi ya ujenzi wa shule sambamba na vituo vya afya katika kata mbalimbali wilayani hapa”.

Na Elizabeth Makemba

Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 94 mpaka kufikia asilimia 98.91 kwa mwaka fedha uliopita wa 2022/2023, makusanyo hayo yatasaidia katika shughuli mbalimbali za Maendeleo katika wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasahuri ya Wilaya ya Kilosa Ndg Kisena Mabuba katika Mkutano wa kawaida wa Baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa FDC Ilonga.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Kilosa ndg Mabuba

Mabuba alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa uliofanyika baina ya waheshimiwa Wabunge, Madiwani, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Watendaji wa halmashauri ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Kilosa ndg Mabuba

“Na ndio mana katika kipindi cha miaka hii miwili tumefanikiwa katika sekta ya elimu tumeweza kuwafikia hata wanafunzi waliokuwa wanatembea umbali mrefu kwa kujenga shule za awali, msingi na sekondari mfano katika kata za Msowero na Mtumbatu” alisema Mkurugenzi Mabuba.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mhe Wilfred Sumari

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred Sumari alisema kuwa maendeleo ya wilaya hiyo yametokana na usimamizi mathubuti wa Mkurugenzi mtendaji na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati unaotakiwa.

Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mhe Sumari
Wakuu wa idara wakifuatilia kikao cha baraza la madiwani

Awali katika Mkutano huo Diwani wa kata ya Magubike Mhe. Abuu Msofe aliapishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mh. Agnes Ringo baada ya kushinda uchaguzi mdogo uliofanyika Julai 13,2023 baada ya diwani aliyekuwa akiongoza kata hiyo kufariki dunia .