Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
25 June 2026, 14:53

Uvunaji wa mazao ya misitu unalenga kuhakikisha rasilimali za misitu zinatumika kwa manufaa ya wananchi na taifa bila kuharibu mazingira na ukichangia kuongeza mapato ya serikali na kuboresha maendeleo ya kijamii.
Na Asha Madohola
Watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji Wilayani Kilosa wametakiwa kusimamia, kuhakiki na kuwajibika kikamilifu katika kulinda mazingira na kuhakikisha misitu haivunwi hovyo ili kuendelea kuwa chanzo cha maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wilaya ya Kilosa, Salome Dismas Mkinga, akimwakilisha Mwenyekiti wa kikao ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kilosa katika kikao cha kujadili na kuhakiki majina ya waombaji wa kuvuna mazao ya misitu kwa msimu wa mwaka 2026/2027, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkinga amesema viongozi wa vijiji wana nafasi kubwa katika kusimamia rasilimali za misitu kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za uvunaji wa mazao ya misitu zinafuatwa ili kuzuia uharibifu wa mazingira huku akisisitiza kuwa usimamizi mzuri wa misitu ni msingi wa uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu ya wananchi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Hilda Mwilongo, amesema mchakato wa kujadili na kupitisha majina ya waombaji wa kuvuna mazao ya misitu ulizingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uhalali wa maombi, maeneo yanayoruhusiwa kuvunwa pamoja na kuzingatia sheria za uhifadhi wa misitu.
Amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha uvunaji unafanyika kwa njia endelevu bila kuharibu rasilimali za misitu na uvunaji wa mazao ya misitu unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na Halmashauri kupitia ongezeko la mapato, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda misitu na kutoa taarifa za vitendo vya uvunaji haramu ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kuwepo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Beatrice Mwinuka, amesema misitu ni rasilimali muhimu inayochangia ukuaji wa uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa “misitu ni fedha” kutokana na mchango wake katika kuongeza mapato ya Halmashauri na kuboresha huduma za jamii pia amewataka watendaji na viongozi wa vijiji kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa katika kikao hicho ili kuhakikisha uvunaji wa mazao ya misitu unafanyika kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za uhifadhi wa mazingira.
