Radio Jamii Kilosa

Tindiga yapokea msaada kufuatia mafuriko

30 April 2026, 15:06

Wananchi wa Tindiga wakipokea misaada ambayo ilikabidhiwa na Katibu Tawala Kilosa Salome Mkinga. Picha Idd Manjawila.

Mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa yamesababisha uharibifu wa makazi, mashamba na miundombinu, na kuwaacha wananchi wengi wa kata ya Tindiga bila makazi na chakula.

Na Beatrice Majaliwa

Shirika la Norwegian Church Aid kwa kushirikiana na Anglican Dayosisi ya Morogoro limetoa msaada kwa waathirika wa mafuriko katika Kata ya Tindiga Wilayani kilosa kufuatia athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa NCA Theonat Mushi akisoma taarifa

Akizungumza wakati wa ugawaji wa msaada huo Kaimu Mkurugenzi wa Norwegian Church Aid Theonat Mushi amesema kuwa lengo ni kuwasaidia wananchi waliopoteza makazi yao kurejea katika hali ya kawaida kwa haraka iwezekanavyo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na mashirika ya misaada na jamii katika kukabiliana na majanga ya asili.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi wa NCA Theonat Mushi akizungumza

Aidha Mushi aliongeza kwa kusema kuwa msaada huo unatakiwa uwafikie waathirika moja kwa moja na miongoni mwa vitu vilivyotolewa ni pamoja na Mablanketi,magodoro,vyandarua,vidonge vya kutibu maji na vichujio vyake ili kuhakikisha afya zinakaa sawa.

Askofu Godfrey Sehaba wa Dayosisi ya Anglikana Morogoro akisoma taarifa

Naye Askofu Godfrey Sehaba wa Dayosisi ya Anglikana Morogoro alisema kuwa wameendelea kujitoa kwa jamii kwa kutoa msaada wa dharura na kulenga kusaidia kaya mia tatu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa ili kuwasaidia kutokana na adha waliyoipata. 

Askofu Godfrey Sehaba wa Dayosisi ya Anglikana Morogoro akizungumza
Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Dismas Mkinga

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Dismas Mkinga akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ametoa shukrani kwa NCA, kanisa la Anglikana na uongozi wa kijiji na Kata kwa kujitoa kwao na kusema kuwa misaada iliyotolewa imetoa faraja kubwa kwa wahanga ambao wamepoteza makazi, mali na vyanzo vya kipato kutokana na mvua kubwa zilizonyesha.

Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Dismas Mkinga akizungumza

Ikumbukwe kuwa waathirika hao waliopatiwa msaada huo ni kutokana na mafuriko yaliyotokea Mwishoni mwa mwaka 2025 ambayo yaliathiri makazi, vyakula,mazao na miundombinu kwa ujumla na jumla ya kaya 382 zenye idadi ya watu 1120 wa kutoka katika kijiji cha Malangali na Tindiga walikumbwa na adha hiyo ya mafuriko ambapo mpaka sasa wapo kwenye makambi hayo maalumu.