Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
4 June 2026, 16:30

Mfumo wa stakabadhi hhalani unalenga kuondoa unyonyaji wa wakulima, kuongeza uwazi katika biashara ya mazao, kuhakikisha matumizi ya vipimo sahihi, na kuwawezesha wakulima kupata malipo yanayolingana na thamani halisi ya mazao yao.
Na Beatrice Majaliwa
Wakulima na viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Msingi vya Masoko ya Kilimo (AMCOS) wilayani Kilosa wametakiwa kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya vipimo sahihi vinavyotambulika kisheria katika biashara ya mazao ili kuimarisha uwazi na kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa ununuzi na uuzaji wa mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Wito huo ulitolewa Juni 3, 2026 na Afisa Kilimo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Musa Masolwa Dominico, alipokuwa akizungumza na viongozi wa Tarafa ya Kilosa Mjini kuhusu umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi katika shughuli za biashara ya mazao. Amesema matumizi ya vipimo vinavyokubalika kisheria ni msingi muhimu wa kuhakikisha haki inapatikana kwa wakulima na wanunuzi, huku yakichangia kuongeza uaminifu katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
Musa amefafanua kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani umeendelea kuwa mkombozi kwa wakulima wengi kwa kuwawezesha kuuza mazao yao kwa bei zenye tija na kuondokana na changamoto za unyonyaji zilizokuwa zikijitokeza katika mifumo ya awali ya masoko. Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya vipimo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha wakulima na kuimarisha maendeleo ya sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kiwili AMCOS, Khalfani Tetema, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo na kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya vipimo katika biashara ya mazao na kwamba viongozi wa AMCOS watahakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa ili kuepusha dosari zinazoweza kumuathiri mkulima na kuhakikisha wakulima wanapata stahiki zao kwa usahihi.

Naye Diwani wa Kata ya Kasiki, Mhe. Ramadhani Mpangachuma, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa kwa kina namna mfumo wa stakabadhi ghalani unavyofanya kazi na faida zake kwa wakulima na ameahidi kuwa balozi mzuri wa kueneza elimu hiyo kwa wananchi na wakulima katika kata yake ili
Mmoja wa wakulima aliyehudhuria katika mafunzo hayo Ally Mdimu amesema kuwa mfumo huo umekuwa ni msaada mkubwa kwa wakulima kwani wanaweza kuhifadhi mazao yao kwa usalama akisubiri mchakato wa mnada ambapo wanunuzi wakipatikana mazao yao yanauzwa kwa uhakika.