Radio Jamii Kilosa

Vijana Kilosa wahimizwa kupinga rushwa

22 July 2026, 11:48

Afisa Takukuru wilaya ya Kilosa Nerry Daud akiwa kwenye studio za Redio Jamii Kilosa akitoa elimu kuhusu rushwa. Picha na Epiphanus Danford

Kupambana na rushwa kunahitaji ushirikiano wa wananchi wote kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi vitendo vya rushwa vinapobainika.

Na Asha Madohola

Jamii, hususan vijana wa Wilaya ya Kilosa, wamehimizwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na badala yake kujenga utamaduni wa uadilifu, uwajibikaji na uaminifu ili kuwa chachu ya maendeleo endelevu katika jamii.

Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kilosa, Nerry Daud, ambaye amesema rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo kwa kuwa hudhoofisha haki, usawa na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Amesisitiza kuwa vijana ni nguvu kazi ya Taifa na viongozi wa baadaye, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupinga vitendo vya rushwa.

Afisa Takukuru Kilosa Nerry Daud akizungumza katika kipindi maalumu

Aliongeza kwa kusema kuwa vijana wanapaswa kuwa mfano mzuri kwa kukataa kutoa au kupokea rushwa katika mazingira yoyote huku akiwahimiza kujituma katika shughuli halali za kujipatia kipato na kufanikisha malengo yao kwa njia zinazokubalika kisheria.

Hata hivyo aliwataka kutoa taarifa TAKUKURU wanaposhuhudia vitendo vya rushwa ili kusaidia kujenga jamii yenye haki, uwazi na uwajibikaji na akatoa wito kwa jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwalea vijana katika misingi ya maadili mema, uaminifu na uzalendo.

Amesema vita dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mwananchi, na ushiriki wa vijana ni nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye maendeleo, haki na ustawi wa kudumu.

Mtangazaji Asha Madohola akiwa katika studio za Redio Jamii Kilosa kwenye kipindi maalumu