Radio Jamii Kilosa

Unyonyeshaji pekee hulinda afya ya mtoto

5 August 2026, 14:08

Afisa Lishe Salha Juma akitoa elimu kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama katika studio za Redio Jamii Kilosa. Picha na Amos Msingi

Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni njia bora ya kumpatia mtoto lishe kamili, kinga dhidi ya magonjwa na msingi mzuri wa ukuaji katika miezi sita ya mwanzo wa ukuaji wake.

Na Asha Madohola

Wananchi Wilayani Kilosa wamehimizwa kuendelea kuzingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wenye umri wa chini ya miezi sita, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yanayoendelea kuanzia Agosti Mosi hadi Saba mwaka huu.

Akizungumza na Redio Jamii Kilosa, Afisa Lishe Salha Juma, alisema maadhimisho hayo yanabeba kauli mbiu isemayo “Mwanzo mzuri wa maisha ya mtoto huanza na maziwa ya mama,” akieleza kuwa maziwa ya mama ndiyo chakula na kinywaji pekee kinachokidhi mahitaji yote ya mtoto katika miezi sita ya kwanza ya maisha.

Salha alisema dhana inayodai kuwa watoto hawashibi kwa maziwa ya mama si sahihi, kwani mara nyingi tatizo linatokana na namna mtoto anavyonyonyeshwa pia amefafanua kuwa mtoto anatakiwa kunyonya ziwa moja hadi lipungue vizuri kabla ya kuhamishiwa kwenye ziwa lingine ili apate maziwa yote muhimu, yakiwemo ya kumkata kiu na yale yenye virutubisho vinavyomshibisha na kumwezesha kukua vizuri.

Afisa Lishe Salha Juma akiwa katika kipindi cha Ijue Halmashauri yako Idara ya Afya

Aidha, amewatahadharisha wazazi na walezi dhidi ya tabia ya kuwapa watoto uji, maji, matunda au vyakula vingine kabla ya kutimiza miezi sita, akieleza kuwa mfumo wa mmeng’enyo wa mtoto katika kipindi hicho haujawa tayari kumeng’enya vyakula hivyo. Amesema kufanya hivyo kunaweza kusababisha matatizo mbalimbali ya afya ikiwemo maumivu ya tumbo, kuvimbiwa, gesi pamoja na kuongeza hatari ya mtoto kupata uzito uliopitiliza na magonjwa yasiyoambukiza akiwa baadaye maishani.

Kwa upande mwingine, Afisa Lishe huyo ametoa wito kwa jamii kuachana na mila na desturi potofu zinazokwamisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama, ikiwemo imani kuwa mtoto apewe vyakula vingine mapema au tabia zinazomnyima mtoto haki ya kunyonya maziwa ya mama ya kutosha huku akisisitiza kuwa watoto wanapaswa kunyonya mara nyingi, angalau zaidi ya mara kumi kwa siku, na kwamba maziwa ya mama ndiyo msingi wa afya, ukuaji na maendeleo bora ya mtoto.