Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
9 September 2024, 23:46

Na Farida Hassan
Vitisho na vipigo ni miongoni mwa sababu kubwa zinazopelekea wanawake wengi nchini kushindwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa na watu mbalimbali katika jamii hususani wenza wao.
Kauli hiyo imetolewa na Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Masanze wilayani Kilosa Bi Amina Mangali wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa wanawake wengi wamekuwa wakifanyiwa vitendo viovu kama vile kupigwa, kubakwa, kulawitiwa pamoja na kutelekezewa watoto lakini hawasemi kwa kuogopa vipigo na kuuawa.
“Wanawake wengi wanapofanyiwa ukatili hutishiwa na kuambiwa wakae kimya na endapo watasema wataongezewa mateso au kupotezwa kabisa hali ambayo inawafanya wakae kimya na kuendelea kufanyiwa vitendo hivyo viovu” alisema Mhe Mangali.
Sanjari na hayo mmoja wa wanawake ambaye ni mmoja wa wahanga wa kufanyiwa vitendo vya ukatili amewaasa wanawake kuwa wepesi kufika sehemu husika kutoa taarifa za vitendo wanavyofanyiwa kwani kufanya hivyo itasaidia wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kukomesha vitendo hivyo.