Radio Jamii Kilosa

Miaka 59 ya Muungano Kilosa yaadhimisha kwa kupanda miti katika mto Mkondoa

27 April 2023, 10:13 am

Mto Mkondoa ulipandwa miti kilele cha Muungano Kilosa. Picha na Idd Manjawila

Viongozi wa kata na vijiji wilayani Kilosa wametakiwa kujiwekea malengo ya upandaji miti kuanzia ngazi ya kata kupanda miti takribani 500 kwa mwezi ili kutimiza azma ya serikali ya kufikisha idadi ya miti milioni moja na nusu kwa mwaka 2022 – 2023.

“Wananchi wametakiwa kufahamu kuwa Muungano umekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya nchi ikiwemo mwingiliano wa kimahusiano baina ya Tanzania bara na visiwani,uendelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na wanayo kazi ya ya kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama tunu ya Taifa ili kulifanya Taifa kuwa lenye umoja na mshikamano”.

Na Asha Madohola

Serikali imewataka wakazi wa Kilosa kuhakikisha wanaacha kufanya uharibifu wa mazingira badala yake wayatunze ilii kuepukana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri uoto wa asili na badala yake kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa mazingira.

Mkuu wa wilaya ya Kilosa akipanda mti

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka kwenye Maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo wilayani Kilosa yaadhimisha sherehe hizo kwa kupanda miti katika mto Mkondoa.

Aidha Mhe. Shaka alisema kumekuwa na tabia ya ukataji miti na kutothamini misitu jambo ambalo si sahihi, hivyo kila mmoja anao wajibu wa kutunza mazingira kwa kufanya jitihada za upandaji miti kuwa zoezi endelevu kwa kuwa hadi sasa wilaya imefanikiwa kupanda miti zaidi ya laki saba kati ya miti 1,500,000 ambayo ni lengo la kitaifa kwa mwaka 2022/2023.

“Tukiwa tunadhimisha miaka 59 ya Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar tumeamua kuunga mkono jitihada za Mhe Rais katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyoikumba dunia na kuleta madhara makubwa kutokana na uharibifu wa vyanzo vya misitu” alisema Mhe Shaka.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka
Katibu Tawala wa wilaya ya Kilosa Mhe Yohana Kasitila akizungumza

Kwa upande wake Katibu Tawala Yohana Kasitila alisema kuwa upandaji miti umefanyika katika mto Mkondoa kwa lengo la kuendeleza utunzaji wa mto huo ili kuondoa adha ya mafuriko ya mara kwa mara na kampeni ya upandaji miti itakuwa endelevu katika mito mingine iliyopo wilayani Kilosa.

Afisa Maliasili wilaya ya Kilosa Sadala Ally akisoma risala

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa upandaji miti Afisa Maliasili Sadala Ally amesema zoezi la upandaji miti kwa wilaya ya Kilosa ni endelevu ambalo linashirikisha wadau mbalimbali na mpaka sasa imeshapanda miti 789,387 na kufikia asilimia 53 ya lengo la kitaifa kwenye upandaji wa miti.

Sauti ya Afisa Maliasili Kilosa Sadala
Wananchi wakiwa mto Mkondoa kwenye zoezi la upandaji miti