Radio Jamii Kilosa

Wakulima watakiwa kulima kilimo cha Ikolojia.

30 January 2023, 1:45 pm

Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa wakulima wilaya ya Kilosa wametakiwa kulima kilimo ikolojia ambacho ni Kilimo rafiki kwa mazingira na kinasaidia kupunguza gharama za kununua madawa na mbolea kwa ajili ya kustawisha mashamba na kuua wadudu kwenye mazao.

Hayo yamebainishwa leo januari 18 2023 na mfanyakazi wa shirika la Action Aid Tanzania ambapo pia ni Msimamizi wa mradi Kitaifa wa kuchochea uwajibikaji na ufanisi katika kilimo Ikolojia na afya Samweli Stanley Mkwatwa ambapo amesema kuwa lengo la mradi ni kuwajengea uwezo wakulima wadogo waweze kujua kilimo rafiki na kuichagiza serikali katika kutoa huduma za ugani

Msimamizi wa mradi wa Kitaifa wa kuchochea uwajibikaji na ufanisi katika Kilimo Ikolojia na Afya akitoa maelekezo na Maafisa Ugani na Viongozi wa Afya Kata Wilayani Kilosa
Msimamizi wa mradi wa Kitaifa wa kuchochea uwajibikaji na ufanisi katika Kilimo Ikolojia na Afya akizungumza na Maafisa Ugani na Viongozi wa Afya Kata Wilayani Kilosa

Aidha Samweli amesema kwa miaka saba ya mradi  wamefanikwa kwa kuihamasisha serikali kutenga bajeti katika kilimo ikolojia ambapo kwa sasa pia wametenga maeneo kupitia vijiji kwa ajili ya mashamba darasa pia halmashauri imetoa nafasi kwa wakulima wadogo wadogo kutengeneza mbegu zao na kuuziana wenyewe.

Mratibu huyo ameongeza kwa kusema kuwa kwenye afya elimu ya uzazi awali vijana balehe walikuwa hawapatiwi elimu ambapo kwa sasa hilo linafanyika na wametengewa muda lakini pia kuna jukwaa la wanawake wakulima wadogo wadogo ambapo wanajadili masuala ya kilimo na kutatua changamoto zinazowakabili.

Hata hivyo ameiomba halmashauri kuendeleza mradi walipoishia kwa kuwawezesha makundi ambayo mradi umewawesha ikiwemo jukwaa la wanawake wakulima wadogowadogo ili waweze kuwanufaisha wengine kwa kuleta maendeleo katika jamii nzima

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji Mkoa wa Morogoro Joseph Renatus Sengasenga katika miaka saba ya mradi wa PSA Mradi Wa Uwajibikaji Jamii walionufaika ni wakulima wanawake na vijana kwakuwa walijengewa uwezo wa kudai haki katika sekta ya kilimo kwenye utolewaji wa huduma za ugani na wakaongeza uzalishaji wenye tija.

Mratibu wa Mradi wa Mtandao wa vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Morogoro Joseph Sengasenga akizungumzia Miaka saba ya Mradi wa PSA.

Sengasenga asema kuwa kwa kushirikiana na halmashauri wameweza kuwajengea uwezo vijiji vitano namna ya kuzalisha mbegu kwa tija kwenye mbegu za asili ambazo zinagharama nafuu lakini zina ubora na kwamba wamewezesha wakulima kupata mbolea katika ujazo mdogo ambayo mkulima mdogo anaweza kumudu kununua hivyo amewataka wakulima kulima kilimo cha ikolojia na kupanda mbegu himilivu zinazostahimili ukame.

Mratibu wa Mradi wa Mtandao wa vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Morogoro Joseph Sengasenga akizungumzia umuhimu wa matumizi ya mbegu za asili.