Radio Jamii Kilosa

Ujenzi wa barabara za kiuchumi wawakuna wakulima Kilosa

9 April 2024, 3:07 pm

Mradi wa barabara ya Ilonga-Mfuluni katika kata ya Chanzuru wilayani Kilosa ukiendelea kutekelezwa. Picha na Kayanda

Serikali imedhamiria kwa dhati kumaliza changamoto za miundombinu ya barabara kwa kutengeneza madaraja, mifereji na makaravati wilayani Kilosa kwa kuondoa adha ya usafiri na kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuweza kusafirisha mazao yao kuyapeleka kwenye masoko makubwa ambayo yatawaongezea kipato mara dufu.

Na Asha Rashid Madohola

Wakulima wa kata za Mbumi na Magomeni wanaolima katika bonde la Kisaki wamenufaika na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara mbili ambapo awali hakukua na barabara maeneo hayo na kusababisha kuzorota kwa shughuli za kiuchumi.

Hayo yamebainika katika ziara ya Mbunge wa jimbo la Kilosa akiwa pamoja na kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Kilosa ambao walifika na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo na kuridhishwa na maendeleo ya mradi ambapo wananchi wanaendelea kuzitumia licha ya kwamba hazijakamilika.

Diwani wa kata ya Magomeni Mchuuzi Limbanga akiongelea mradi wa barabara

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya hiyo Bi Fatuma Saidi na diwani wa kata ya Magomeni Mchuuzi Limbanga wameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi wa barabara ambapo imeshachongwa umbali wa kilomita moja na wananchi itawanufaisha kiuchumi kwa kuwa wanategemea kilimo kukuza kipato chao.

Sauti ya mwananchi na diwani kata ya Magomeni
Mradi wa ujenzi wa mfereji ukiendelea katika kata Mbumi

Aidha ziara hiyo ilifika kukagua mradi wa ujenzi wa mfereji wenye urefu wa mita 450 unaogharimu shilingi milioni 200 ambapo mkandarasi wa mradi kupitia kampuni ya Kupala Works Bi Mary Sanga na Meneja wa Tarura wilayani Kilosa Winston Mnyaga wamesema hali ya mradi inaendelea vizuri changamoto iliyopo na hali ya hewa ya mvua ndio inachelewesha ukamilishaji wa mradi.

Sauti ya mkandarasi na Meneja Tarura wilaya ya Kilosa
Katibu wa CCM wilaya ya Kilosa Shaban Mdoe

Kwa upande wake Katibu wa CCM Shaban Mdoe alisema ziara hiyo imekua ya mafanikio makubwa kwa kuwa wamekagua na kuziona changamoto ila miradi yote inaendelea vizuri na hivi karibuni wananchi watanufaika na miradi hiyo.

Sauti ya katibu wa CCM Shaban Mdoe
Mwenyekiti wa Halmashauri Wilfred Sumari akizungumza

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Wilfred Sumari alishukuru kata yake kupelekewa mradi wa barabara kuanzia Ilonga hadi Mfuluni na kuomba serikali kuzimalizia kilometa tatu ili ifike Kijiji cha Idete na kuwanufaisha wananchi wa huko.

Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri Wilfred Sumari
Wakazi wa Rudewa wakizungumza kero ya barabara

Hata hivyo wakiwa katika kata ya Rudewa wananchi waliiomba serikali kuwaondolea adha ya barabara ya kutoka Tembeni hadi Peapea kwa kuwa kipindi cha mvua haipitiki huku ng’ombe wakiwa kero katika kuharibu miundombinu hiyo.

Sauti za wakazi wa Rudewa

Kwa upande wake Mbunge Prof Palamagamba Kabudi aliishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Hassan kwa kulipatia jimbo la Kilosa fedha nyingi za kuwaletea wananchi miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara na kuwataka wananchi wawe na imani na serikali yao kwa kuwa maendeleo yatawafikia wote.

Sauti ya Mbunge Prof Kabudi akizungumza