Radio Jamii Kilosa

Ujenzi tuta la mto Mkundi latumia milioni 30 kuzuia mafuriko Dumila

6 April 2024, 10:04 pm

Mto Mkundi ambao umekua ukisababisha mafuriko kata ya Dumila. Picha na Yusuph Kayanda

Kutokana na mafuriko ya mara kwa mara yanayotokea wilayani Kilosa hususani katika kata ya Dumila na kupelekea kuathiri shughuli za kiuchumi serikali imedhamiria kumaliza changamoto hiyo kwa kutenga fedha zitakazotumika katika ujenzi wa tuta ambalo litakuwa suluhisho.

Na Asha Madohola

Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi alifanya ukaguzi wa ujenzi wa tuta la kuzuia maji yanayotapika nje ya mto Mkundi uliopo kata ya Dumila wilayani Kilosa na kusababisha mafuriko katika makazi ya watu wanaoishi pembezoni mwa mto huo na kusababisha athari za uharibifu wa mali na kuhatarisha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza

Akiongozana na Diwani wa kata ya Dumila Douglas Mwigumila, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi katika kata Saburi Sabuni, Mratibu wa shughuli za Jimbo Everist Msakila na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na usalama kata hiyo ambapo Prof, Palamagamba Kabudi aliwasisitiza wananchi wanaoishi pembezoni mwa mto huo kuacha kufanya shughuli za kilimo pembezoni mwa mto ili kuzuia uharibifu unasababisha mto huo kutoroka katika mkondo wake.

Ujenzi wa kujenga tuta hilo la udongo pamoja na juhudi za kuchimbua mto Mkundi ulitokana na athari za Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kusababisha mafuriko katika maeneo ya makazi ya watu hali iliyosababisha uharibifu wa mali pamoja kuhatarisha usalama wa wananchi.

Aidha Prof, Kabudi alitoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa hatua Madhubuti alizochukua kwa wakazi wa Kilosa waliokumbwa na mafuriko katika kata za Kidete, Mamboya, Dumila kutokana na mto huu Mkundi, Msowero, Mvumi, Rudewa, Mkwatani, Kimamba ‘A’.

“Hapa tuliposimama mto ulihama njia yake na kuingia katika eneo la msufini na kusababisha madhara makubwa, tulichokifanya hapa ni hatua za awali ili kudhibiti mafuriko yasifike katika makazi ya wananchi, ambapo gharama za kuchambua na kuweka tuta uligharimu zaidi ya milioni 30” alisema Prof, Kabudi.

Sambamba na hayo Prof, Kabudi alitoa shukrani za dhati kwa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi chini ya Mtendaji Mkuu wa Kiwanda hicho kwa kutoa mtambo uliotumika kuchimbua mto na kupandisha tuta litakalosaidia kutuzuia mafuriko kufika katika makazi ya wananchi.

Nao baadhi ya Wananchi waliohudhuria kujionea ujenzi wa tuta hilo walidai kukamilika kwa tuta hilo kumeweza kuwasaidia kutopata madhara ya mafuriko kwa mvua kubwa iliyonyesha (Aprili 4, 2024) kwani kwa ukubwa wa mvua hiyo ungeweza kuleta mafuriko katika makazi ya wananchi.

Mbunge Prof Kabudi akiwa na viongozi mbalimbali katika ukaguzi wa tuta mto Mkundi