Radio Jamii Kilosa

Prof Kabudi azindua rasmi mashindano ya Moruwasa Ramadan Cup 2024 Kilosa

8 March 2024, 11:29 pm

Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof Kabudi katikati na baadhi ya viongozi kutoka taasisi mbalimbali. Picha na Asha Madohola

Maji safi na salama ni afya kwa binadamu, kwa kutambua umuhimu wa hilo Moruwasa Kilosa imeamua kuandaa ligi ya mpira wa miguu ili kuwakutanisha Jamii na kuipatia elimu juu ya utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji.

Na Asha Madohola

Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe. Prof Palamagamba Kabudi leo ameyazindua Rasmi Mashindano ya Mpira wa Miguu ya MORUWASA RAMADHANI CUP 2024 yenye dhamira ya kuisogeza Jamii kwa pamoja kupata burudani sambamba na ujumbe kutoka taasisi mbalimbali kama falsafa ya Moruwasa ikisema maji ni uhai tunza mazingira na vyanzo vya maji.

Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof Kabudi akizungumza

Mhe Prof. Kabudi aliwapongeza Moruwasa pamoja na wote walioandaa Mashindano hayo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutunza vyanzo vya Maji na kulinda miundombinu ya Maji pamoja na kutokuharibu miundombinu ya umeme kwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo kutokana na kukatikakatika kwa umeme ili kupisha matengenezo.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozaa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inayodhamira ya dhati ya kumaliza changamoto ya umeme hivi karibuni lakini kuna baadhi ya watu wanaihujumu miundombinu ya umeme hususan kwenye matransfoma wanaiba mafuta ambayo yanatumika kupikia ni hatari kwa afya” alisema Prof Kabudi.

Prof Kabudi akiwakabidhi zawadi manahodha wa timu zote mbili

Mashindano ambayo yatahusisha Timu 12 yaliyodhaminiwa na Moruwasa Wilaya ya Kilosa, baada ya yakufunguliwa Rasmi mapema hii leo kwa mchezo wa Ngao ya Hisani uliozikutanisha Timu ya Polisi Fc na Timu ya Kilosa Talent Academy ambazo kwa dakika tisini za mchezo zimetoshana nguvu kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana na kukabidhiwa zawadi za mpira mmoja kila timu na pesa taslimu

Meza Kuu wakifuatilia mpira katika viwanja vya shule ya msingi Kichangani
Manahodha wakifurahia baada ya kukabidhiwa zawadi na Prof Kabudi