Radio Jamii Kilosa

Watumishi watakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za serikali

29 March 2024, 5:06 pm

Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Michael John Gwimile akizungumza na watumishi. Picha na kitengo cha habari serikalini

Ili kuleta kasi ya maendeleo kwa wananchi wote watumishi inatakiwa waendane sambamba na miongozo ya kiserikali ya kiutendaji ambayo ndio itakua chachu pekee ya kuleta maendele.

Na Asha Rashid Madohola

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg Michael John Gwimile amewataka Watumishi wote kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia kanuni, Sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali lengo likiwa ni kuwaletea maendeleo Wananchi kama ilivyokusudiwa.

Aliyasema hayo wakati wa kikao chake na Watumishi wa Divisheni na vitengo vyote kutoka Makao Makuu ya Halmashauri, kikiwa na lengo la kujitambulisha rasmi na kukumbushana masuala mbalimbali ya kiutumishi huku akisititiza nidhamu, itifaki ya mawasiliano kazini, pamoja na haki na wajibu wa mtumishi.

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa wakifuatilia kikao.

“Kila mtumishi anapaswa kuzingatia Sheria,Taratibu na kanuni zilizowekwa na Serikali hiyo itasaidia katika kukuongoza kufanya masuala mbalimbali pindi unapokuwa katika kutimiza majukumu yako,” alisema Mkurugenzi Gwimile.

Aidha alisisitiza kuwa kila mtumishi kwa nafasi yake kusimamia taratibu zilizowekwa na kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea Wananchi maendeleo.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Utawala na usimamizi wa Rasilimali watu Ndg Betuely Joseph Ruhega alisema kuwa kutokana na wimbi la watumishi wanaostaafu Utumishi wa Umma kujikuta katika changamoto mbalimbali za kimaisha hususan za kiuchumi hali inayopelekea kupata maradhi au hata kufa hivyo amewaasa watumishi kujiandaa kustaafu mara tu wanapoanza safari yao ya ajira.

“Mtumishi ukijiandaa mapema kiuchumi na kijamii suala la kustaafu kwa namna yoyote ile halitakusumbua hivyo watumishi jifunzeni kuweka akiba na kuacha tabia ya kutegemea chanzo kimoja cha mapatao kwani hiyo inapelekea watumishi wengi kuishi maisha ya kubahatisha,” alisema ndg Ruhega.

Aidha aliwataka watumishi kutafuta vyanzo vingine vya mapato tofauti na mshahara ili hata wanapomaliza utumishi wao Serikalini tayari wanakuwa wameshajikita katika jambo Fulani na hii itawaepushia kukurupuka kuingia kwenye biashara wasizokuwa na uzoefu nazo na kupelekea kuanguka kiuchumi na wakati mwingine kuwasababishia msongo wa mawazo au vifo vya mapema