Radio Jamii Kilosa

Wanafunzi Mazinyungu kufanyiwa uchunguzi wa macho, masikio

7 May 2024, 11:46 am

Mwaliku Mkuu Msaidizi wa shule ya msingi Mazinyungu akitoa taarifa ya upimaji macho na masikio. Picha na Asha Mado

Serikali imedhamiria kuondoa tatizo la uoni hafifu na kutokusikia kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini kwa kuweka mpango madhubuti wa kuwapima macho na masikio wanafunzi wote na watakaobainika waweze kupatiwa matibabu mapema ili isiwaathiri katika usomaji wao.

Na Asha Rashid Madohola

Wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma katika shule ya msingi Mazinyungu iliyopo kata ya Kasiki wilayani Kilosa mkoani Morogoro wametakiwa kushirikiana na serikali katika kupambana na matatizo ya kiafya yanayoweza kuwakabili watoto.
Hayo yalibainishwa na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya msingi Mazinyungu Ally Mpulu wakati akitoa taarifa kwa wazazi juu ya zoezi la upimaji wa macho na masikio linaloendelea kwa wanafunzi kuanzia darasa awali hadi la nne shuleni hapo.
Mwl Mpulu alisema kuwa serikali imekuja na mpango wa kupima wanafunzi macho na masikio ili kubaini kama wana matatizo watibiwe kwa haraka na isiwe chanzo cha kutofaulu na kushindwa kutimiza ndoto zao.

Hata hivyo ameishukuru serikali kwa jitihada hizo za kupambana na matatizo ya kiafya kwa wanafunzi na kuweza kugharamia matibabu endapo watatokea watoto wenye matatizo hayo.

Sauti ya Makamo wa shule ya msingi Mazinyungu Mwl Ally Mpulu
Hosea Mgunda mzazi wa mwanafunzi anayesoma shule ya msingi Mazinyungu

Awali wakizungumza na Redio Jamii Kilosa baada ya kupokea taarifa za upimaji wa wanafunzi, wazazi na walezi waliishukuru serikali kuwaletea mpango huo wa kuwanusuru watoto na tatizo la usikivu na uoni hafifu kwani utawasaidia kubaini matatizo ya watoto na kuyatibia na kuwaomba walimu kupatiwa taarifa za mapema kabla ya kuanza kutekelezwa kwa maagizo ya serikali.

“Sisi kama wazazi tumeipokea vizuri taarifa ya serikali ya kuamua kuwapima watoto wetu kwa lengo la kubaini changamoto za usikivu na uoni ila tunawaomba walimu wawe wanatushirikisha wazazi kabla hawajaanza zoezi” alisema mmoja wa wazazi

Sauti za wazazi wa wanafunzi shule ya msingi Mazinyungu