Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
9 September 2024, 19:20

Waandishi wa habari wanawake wameziomba mamlaka husika kutambua mchango wao katika tasnia ya habari nchini yenye dhumuni la kuihabarisha jamii katika masuala mbalimbali kama vile ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ili kuchagiza chachu ya maendeleo kupitia uhabarishaji.
Na Asha Madohola
Imeelezwa kuwa rushwa ya ngono katika maeneo mengi imekuwa moja ya sababu kubwa kwa waandishi wa habari wanawake kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kushindwa kupata habari katika chanzo husika.
Hayo yalibainishwa na baadhi ya waandishi wa habari wanawake wakati wakizungumza na Redio Jamii Kilosa ambapo wamesema kuwa jinsia yao ya kike imekuwa ikiwanyima uhuru katika kutaka uwiano kwenye habari kwa kuwa mhusika hushindwa kutoa ushirikiano baada ya kunyimwa rushwa ya ngono.

Akizungumza na kituo hiki, Beatrice Majaliwa amesema kuwa wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi katika mahali pa kazi na kupelekea kushindwa kujiamini huku wengine wakijirahisisha wenyewe kwa wahusika na kushindwa kukataa pindi wanapoombwa rushwa ya ngono ili kupata habari kutokana na maslahi madogo wanayolipwa wanapofanyia kazi.
“Mara nyingi waandishi wa habari wanawake tumekuwa tukijirahisisha kwa wadau na kupelekea kuombwa tutoe rushwa ya ngono ili tuweze kupata habari na hii ni kutokana pia na malipo madogo tunayolipwa mahala pa kazi hivyo tunaiomba serikali itusaidie” alisema Beatrice.

Kwa upande wake Felister Mbwasi alisema kuwa kuna baadhi ya jamii na mahali pa kazi imeshindwa kuelewa mwandishi wa habari mwanamke anaweza kufanya kazi sawa na mwandishi mwanaume hali ambayo imekuwa ikiwabagua katika utendaji kazi wao hivyo amaeiomba mamlaka husika kuhakikisha wanaweka usawa ili kuweza kuaminika.
Hata hivyo waandishi wa habari kwenye suala la kipato bado ni changamoto, wamiliki wa vyombo vya habari wameshauriwa kuboresha huku wakiomba kufanyike pia maboresho ya sera, sheria ndani ya vyombo hivyo ili ziwe jumuishi kwa wote.