Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
8 July 2026, 12:55

Pichani Ofisi ya Chama Kikuu cha Ushirika Kilosa co-operativu union (KICU). Picha na Epiphanus Danford
Chama hicho kinakwenda kuongeza tija kwa Wakulima wake katika kuhakikisha wanapata huduma bora lakini pia kuhifadhi mazao yao katika maghala yaliyoboreshwa.
Na Epiphanus Danford
Chama Kikuu cha Ushirika Kilosa (KICU) kimeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuimarisha huduma kwa wanachama na wakulima baada ya kukamilisha maboresho makubwa ya ofisi zake pamoja na maghala yanayotumika kuhifadhi mazao, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za ushirika na kuboresha mazingira ya kazi.

Pichani Maghala yaliyoboreshwa na chama kikuu cha Ushirika Kilosa (KICU). Picha na Epiphanus Danford
Akizungumza wakati wa kutembelea maboresho hayo, Mwenyekiti wa KICU, Yegela Jikililo, amesema maendeleo yaliyofikiwa ni matokeo ya juhudi za uongozi wa chama pamoja na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya ushirika nchini.
Yegela amesema kuwa maboresho ya ofisi na maghala hayo yameongeza hadhi ya chama, yameimarisha usalama wa mazao ya wakulima na yameboresha utoaji wa huduma kwa wanachama, huku yakitoa mazingira bora kwa watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Sauti ya mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Kilosa (kicu)
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa KICU bwana Makelemo Mahango amesema chama hicho tayari kimeandaa mpango mkakati wa maendeleo wa miaka mitano ijayo wenye lengo la kukifanya chama kuwa imara zaidi kiuchumi na kuongeza manufaa kwa wanachama wake.
Amesema katika kipindi hicho, KICU kinakusudia kujenga kiwanda cha kukoboa mpunga pamoja na kujenga duka la pembejeo pamoja na kuweka wakala wa huduma za kifedha na kuboresha kiwanda cha pamba kilichopo Kata ya Magomeni Wilaya ya Kilosa.
Sauti ya Meneja wa chama kikuu cha Ushirika Kilosa (kicu)
Meneja Mkuu amesema KICU itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha malengo yote yaliyowekwa katika mpango mkakati huo yanafikiwa kwa wakati na kuifanya Kilosa kuwa mfano wa mafanikio katika sekta ya ushirika nchini.