Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
5 June 2026, 17:42

Wananchi wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na salama kwa mazingira kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu inayohamasisha uwajibikaji katika uhifadhi wa mazingira.
Na Asha Madohola
Wilaya ya Kilosa imeungana na mataifa mbalimbali duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira katika Shule ya Sekondari Chanzuru, Kata ya Chanzuru. Maadhimisho hayo ya kiwilaya yamehusisha upandaji wa miti, uzinduzi wa klabu ya mazingira pamoja na utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi na wananchi, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu inayosisitiza uwajibikaji katika kuijenga Tanzania ya kijani kuelekea mwaka 2050.

Akizungumza mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Afisa Tarafa wa Kimamba, Sabina Lucas Sugwa, alisema kuwa katika wiki ya mazingira duniani wilaya imefanikiwa kupanda miche 40 ya miti ya matunda na miche 160 ya miti ya mbao katika eneo la Shule ya Sekondari Chanzuru na uzinduzi wa Klabu ya Mazingira shuleni hapo utasaidia kuwajengea wanafunzi uelewa na ushiriki wa moja kwa moja katika shughuli za uhifadhi wa mazingira pia serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha vyanzo vya maji, misitu na maeneo ya taasisi yanatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Kilosa, Deus Kijanju, alisema maadhimisho hayo yamekuwa na umuhimu mkubwa kwa kuwa yamehusisha wanafunzi ambao ni msingi wa kizazi kijacho katika juhudi za uhifadhi wa mazingira. Alisema upandaji wa miti pekee hautoshi bila kuwepo kwa utunzaji wa miti hiyo na misitu iliyopo, akisisitiza kuwa wananchi wote wanapaswa kushiriki katika kulinda misitu ya hifadhi, misitu ya vijiji na vyanzo vya maji ili viendelee kutoa manufaa ya kiuchumi, kiafya na kijamii kwa jamii.

Kwa upande wake, Afisa Misitu wa Wilaya ya Kilosa, Sadala Hassan Ally, alisema wilaya imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya serikali inayolenga kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali za mazingira, hususan katika maeneo ya misitu na mabonde huku akisema Kilosa ina misitu 41 ya vijiji na kwamba ushirikiano kati ya serikali na wananchi umeendelea kuwa chachu ya mafanikio katika uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji.

Awali kisoma risala kwa niaba ya wanafunzi na wananchi, Janeth Mussa Mazengo alisema katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Chanzuru, wilaya imefanikiwa kupanda miti 40 ya matunda na miti 160 ya mbao, hatua inayolenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuongeza uoto wa asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

