Radio Jamii Kilosa

TAFIDA Kilosa yasaka vipaji vya waigizaji

26 July 2026, 15:33

Picha ya pamoja ya wasanii Kilosa walioshinda usaili wa waaigizaji wakiwa na viongozi mbalimbali. Picha Asha Madohola

Sanaa ni chanzo halali cha ajira na maendeleo kwa vijana na jamii kwa ujumla na kupitia uigizaji, muziki, uchoraji, uchekeshaji na fani nyingine za sanaa, vipaji vinaweza kugeuzwa kuwa kazi zinazozalisha kipato na kujenga maisha bora.

Na Asha Madohola

Vijana Wilayani Kilosa wamehimizwa kuitumia sanaa kama nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii, kujiajiri na kuelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.

Wito huo ulitolewa wakati wa usaili wa kusaka vipaji vya waigizaji (Audition) ulioandaliwa na Chama cha Waongozaji Filamu Tanzania (TAFIDA) wilaya ya Kilosa uliofanyika katika ukumbi wa Kilosa Club na uliobebwa na kaulimbiu isemayo “Sanaa ni Ajira, Okoa Kipaji Chako.”

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilosa (OCS) Donate Mhina

Mgeni mualikwa katika shughuli hiyo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilosa (OCS) Donate Mhina, amesema sanaa ina nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye amani na mshikamano kwa kuelimisha wananchi kuhusu athari za migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kuhimiza utunzaji wa amani, pamoja na kuhamasisha wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu pia wasanii wana uwezo wa kufikisha ujumbe kwa urahisi na kugusa hisia za jamii, hivyo wanapaswa kutumia vipaji vyao kwa manufaa ya taifa.

Sauti ya OCS Mhina akizungumza
Jaji Mkuu wa mashindano ya waigizaji Kilosa

Akizungumza mara baada ya zoezi la usaili, Jaji Mkuu wa mashindano hayo Khalifan Ahmed (Director Calvin), aliwataka washiriki ambao hawakufanikiwa kufuzu kutokata tamaa, akieleza kuwa kila kipaji kina muda wake wa kung’ara huku akiwasisitiza kuendelea kujifunza, kufanya mazoezi na kujiamini kwa kuwa tasnia ya uigizaji bado inawahitaji vijana wenye ari, nidhamu na ubunifu ili kuendelea kukuza sekta ya sanaa nchini.

Sauti ya Jaji Mkuu Director Calvin akizungumza
Juma Malikila Katibu wa chama cha waigizaji mkoa wa Dar es salaam

Kwa upande wake Juma Malikila Katibu wa chama cha waigizaji mkoa wa Dar es salaam alisema kuwa walioshindwa na kushinda wote ni wasanii hivyo kila mmoja kwa nafasi yake asikate tamaa na kuahidi kwamba katika msimu ujao wa kuandaa kazi zingine wilayani Kilosa watawachukua ili waweze kukuza vipaji vyao.

Sauti ya Juma Malikila akizungumza
Mwenyekiti TAFIDA mkoa wa Morogoro Abdulaziz Babu

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAFIDA Mkoa wa Morogoro Abdulaziz Babu amewapongeza washiriki wote kwa kujitokeza na kuonesha vipaji vyao. Amesema hata wale waliofanikiwa kuchaguliwa wanapaswa kuongeza juhudi, maarifa na ubunifu kwa kuwa sanaa si burudani pekee bali ni biashara na ajira inayoweza kubadilisha maisha na amewatia moyo washiriki ambao hawakuchaguliwa kwa kuwaahidi kuwashirikisha katika fursa nyingine zijazo, huku akiwahimiza vijana wengi zaidi kuamini vipaji vyao na kuvitumia kujiletea maendeleo binafsi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Sauti ya Mwenyekiti TAFIDA Morogoro Abdulaziz Babu akizungumza

Awali akizngumza Afisa Utamaduni wilaya ya Kilosa Christina Massawe aliwataka wasanii walijitokeza kutumia fursa hiyo adhimu ya kuonesha vipaji vyao huenda ndio ikawa mwanzo mzuri wa safari ya mafanikio katika sanaa yake.

Sauti ya Afisa Utamaduni wilaya ya Kilosa akizungumza
Majaji wakiteta jambo