Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
23 September 2026, 15:01

Jamii imetakiwa kuimarisha afya kwa kula vyakula vya asili na kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na mafuta, ili kujenga afya bora na kuzuia changamoto za kiafya zinazoweza kuchangiwa na ulaji usio sahihi.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Kilosa, Elisha Kingu, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa iko tayari kuanza utekelezaji wa shughuli za Wiki ya Lishe Kitaifa, inayotarajiwa kuanza Oktoba 26 hadi 30, 2026, kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na kuhamasisha wananchi kuzingatia ulaji unaosaidia kuimarisha afya.
Akizungumza na Redio Jamii Kilosa, Kingu alisema katika kipindi hicho watafikia makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo akinamama na baba lishe, kwa kuwapatia elimu kuhusu namna ya kuandaa na kutoa vyakula vyenye lishe bora pia elimu hiyo inalenga kuwajengea uelewa wananchi kuhusu uchaguzi sahihi wa vyakula na umuhimu wa kuzingatia lishe katika maisha ya kila siku.

Aidha, alisema kuwa shughuli za Wiki ya Lishe zitatekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni na vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo wataalamu wataendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya lishe, hususan kwa watoto, wazazi na makundi mengine yenye uhitaji wa huduma na ushauri wa lishe.
Kingu alisema maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Imarisha Afya, Kula Kiasili; Punguza Chumvi, Sukari na Mafuta,” inayosisitiza umuhimu wa jamii kutumia vyakula vya asili na kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na mafuta mengi huku akihamasisha wananchi wa Kilosa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika shughuli za Wiki ya Lishe, kusikiliza elimu itakayotolewa na kuanza kutekeleza mabadiliko chanya katika ulaji wa kila siku, kwa kuwa afya bora huanzia kwenye uchaguzi sahihi wa chakula kwa mtu binafsi na familia.