Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
8 September 2026, 12:58

Picha ni Maafisa wa TRA Mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Kilosa wakiwa pamoja kwenye ofisi ya TRA wilaya ya Kilosa. Picha na Epiphanus Danford
Utekelezaji wa sheria ni msingi wa maendeleo kwa uchumi wa taifa letu
Na Aloycia Mhina
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa semina kwa wafanyabiashara wilayani Kilosa mkoani Morogoro, ikiwa na lengo la kuwapatia elimu kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Meneja wa TRA Wilaya ya Kilosa, Bi. Saada Mtoto, amesema lengo kuu la semina hiyo ni kujenga uchumi imara, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza matumizi ya teknolojia pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Amesema elimu hiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara ili kuwawezesha kufahamu mabadiliko mbalimbali ya sheria za kodi na namna yanavyopaswa kutekelezwa katika shughuli zao za kila siku.

Picha ni Meneja wa TRA Wilaya ya Kilosa Bi. Saada Mtoto akizungumza na Wafanyabiashara.
Sauti ya Meneja wa TRA Wilaya ya Kilosa Bi. Saada Mtoto akizungumza na Wafanyabiashara
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi kutoka Morogoro, Bi. Immaculate Chaggu, amewashukuru wafanyabiashara kwa kuitikia kwa wingi wito wa kushiriki semina hiyo.
Bi. Chaggu amesema semina hiyo inalenga kuwakumbusha wafanyabiashara kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka 2026/2027, huku akiwataka kuwa na usikivu wa kutosha ili waweze kuelewa elimu inayotolewa na mamlaka hiyo.

Picha ni Afisa mwandamizi wa huduma na elimu kwa walipa kodi Mkoa wa Morogoro Bi. Immaculate Chaggu akizungumza na Wafanyabiashara wa Kilosa.
Sauti ya Afisa mwandamizi wa huduma na elimu kwa walipa kodi Mkoa wa Morogoro
Naye Afisa Elimu kwa Walipa Kodi na Mawasiliano kutoka Iringa, Bwana Shaga James Gagunda, amesema Serikali kila mwaka huboresha sheria za kodi ili ziendane na dhima ya bajeti na mahitaji ya wakati.
Amesema katika maboresho hayo, baadhi ya vifungu vya sheria za kodi vimeondolewa, huku mabadiliko mengine yakifanyika kwa lengo la kuendana na utekelezaji wa bajeti ya Serikali.

Picha ni Afisa elimu kwa walipa kodi na Mawasiliano Bwana Shaga Gagunda akiwasilisha mada kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Kilosa
Baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki semina hiyo wameishukuru TRA kwa kuwapatia elimu hiyo, wakisema imewasaidia kupata uelewa kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi na wajibu wao kama walipa kodi.
Wameiomba TRA kuendelea kutoa semina na elimu kama hiyo mara kwa mara ili kuwasaidia wafanyabiashara kuendelea kufahamu sheria na taratibu za kodi na hivyo kuepuka makosa yanayoweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi.

Picha ni baadhi ya Wafanyabiashara wakiwa katika mafunzo ya mabadiliko ya sheria za kodi mwaka 2026/2027

Picha ni baadhi ya Wafanyabiashara wakiwa katika mafunzo ya mabadiliko ya sheria za kodi mwaka 2026/2027