Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
26 August 2026, 00:37

Polisi Jamii ni mfumo unaolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kuzuia na kupambana na uhalifu, kudumisha amani na usalama katika maeneo wanayoishi.
Na Asha Madohola
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilosa limehitimisha kilele cha Wiki ya Polisi Jamii kwa kuchangia unit saba za damu salama katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, ikiwa ni sehemu ya matendo ya huruma yaliyofanywa wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii nchini. Shughuli hiyo imefanyika Agosti 25, 2026, kabla ya sherehe za kilele zilizofanyika katika Chuo cha Ualimu Ilonga.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha wiki hiyo, mgeni ramsi katika hafla hiyo, Mkuu wa Polisi Kilosa SSP Janet Bernard Nganda, amesema Wilaya ya Kilosa imeanza shughuli za Wiki ya Polisi Jamii tangu Agosti 19, 2026, kupitia elimu kwa jamii, matendo ya huruma na michezo, huku akieleza kuwa uchangiaji wa damu ni sehemu ya mipango ya kuendelea kuwasaidia wananchi.

Aidha alisema kuwa Polisi Jamii imeleta mafanikio makubwa kwa kuwasogezea wananchi huduma za kipolisi kupitia askari kata na kuimarisha upatikanaji wa taarifa za uhalifu huku akisisitiza umuhimu wa amani, usalama na umoja wa kitaifa na kuwataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi.
Akizungumza kuhusu mchango wa damu uliotolewa na Jeshi la Polisi Kilosa ,Daktari Thomas, mtaalamu wa maabara katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, amewashukuru askari hao kwa kuchangia unit saba za damu, akisema damu hiyo inaweza kusaidia wagonjwa kadhaa kulingana na mahitaji yao, hususan watoto na kwamba hospitali ina mahitaji makubwa ya damu na kuwataka wananchi, taasisi na makundi mbalimbali kuendelea kujitokeza kuchangia damu.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Kituo cha Polisi Kilosa, OCS Donati Mhina, alisema maadhimisho hayo yamekuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kudhibiti uhalifu na kudumisha amani huku akisisitiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati, akieleza kuwa taarifa sahihi zinazotolewa mapema husaidia Jeshi la Polisi kuchukua hatua kabla madhara hayajatokea.
Aidha, amesema elimu ya Polisi Jamii imetolewa kwa makundi mbalimbali, wakiwemo walimu, madereva na wananchi, pamoja na kutumia vyombo vya habari na mikutano ya kijamii na kwa ujumla maadhimisho hayo yameendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Polisi na jamii katika kuimarisha amani, usalama na umoja wa kitaifa.

