Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
3 August 2026, 17:04

Chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa kimefanya Mahafali ya 23 ambapo kimeendelea kudumisha ufaulu wa asilimia 100 kwa miaka mitano mfululizo licha ya kukabiliwa na changamoto za miundombinu na uhaba wa vifaa vya TEHAMA.
Na Asha Madohola
Wahitimu wa Chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa wamehimizwa kutumia taaluma waliyoipata kutoa huduma za afya kwa weledi, maadili na kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza katika Mahafali ya 23 ya chuo hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa, Katibu wa CCM Wilaya ya Kilosa, Janus Mfaume, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu na kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi huku akiwataka wahitimu kuendelea kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya na kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika sekta hiyo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Maafisa Tabibu Kilosa Philipo Mpangala alisema jumla ya wahitimu 62 wamekamilisha mafunzo yao katika Mahafali ya 23 na kueleza kuwa chuo kimeendelea kudumisha ufaulu wa asilimia 100 kwa miaka mitano mfululizo, huku kikikabiliwa na changamoto za ufinyu wa miundombinu, ukosefu wa maabara ya kisasa ya kompyuta na uhaba wa vifaa vya TEHAMA vinavyohitajika katika kufundishia na kujifunzia.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi ambaye ni Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Kilosa, Kilo Mkota, alisema Benki ya NMB itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu na maendeleo pale inapowezekana, huku akiahidi kuzifikisha changamoto zilizoainishwa na uongozi wa chuo katika mamlaka husika ndani ya taasisi hiyo ili ziweze kufanyiwa kazi huku akitoa wito kwa taasisi za fedha, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono jitihada za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika chuo hicho.

Naye mwakilishi wa wazazi Lukindo Korein aliushukuru uongozi wa chuo kwa malezi na elimu waliyoitoa kwa wahitimu hao, huku akiwataka kutumia taaluma yao kwa uadilifu, kuwahudumia wananchi kwa moyo wa kujituma na kuwa mabalozi wema wa taaluma ya afya katika maeneo watakayopangiwa kufanya kazi.
