Radio Jamii Kilosa

Upungufu wa damu uzuilike kwa lishe 

14 September 2026, 12:32

Mtaalamu wa Lishe Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Jackson Kalibwani Picha na Asha Madohola

Jamii imetakiwa kuifanya lishe bora kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, kwa kuchagua na kuandaa vyakula vyenye virutubisho muhimu, kwani afya bora huanza na chakula bora.

Na Asha Madohola

Wananchi wilayani Kilosa wametakiwa kuongeza matumizi ya vyakula vyenye madini chuma katika familia, hususan kwa watoto na wanawake wajawazito, ili kujenga jamii yenye afya bora na yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Wito huo ulitolewa na Mtaalamu wa Lishe kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Jackson Kalibwani, wakati akihitimisha mafunzo kwa Watoa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii, CHW, yaliyowahusisha watoa huduma kutoka vijiji vya kata za Lumuma, Kidete na Uleling’ombe.

Kalibwani alisisitiza umuhimu wa jamii kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao, ikiwemo mboga za majani na vyakula vingine vyenye madini chuma, huku akiwataka wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanapata lishe bora.

Sauti ya Mtaalamu wa lishe Jackson Kalibwani

Aidha aliongeza kwa kusema kuwa maharage makavu yanapaswa kulowekwa kwa zaidi ya saa nane kabla ya kupikwa, huku elimu hiyo ikiendelea kutolewa na CHW kwa jamii ili kuhamasisha ulaji sahihi wa vyakula na kujenga kizazi chenye afya.

Sauti ya Mtaalamu wa lishe Jackson Kalibwani
Juma Selemani Punda mmoja wa washiriki wa mafunzo

Kwa upande wake, Juma Selemani Punda mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, aliishukuru timu ya wataalamu kwa kuwapatia elimu ambayo alisema imewajengea uwezo wa kuwafikishia wananchi maarifa sahihi kuhusu lishe na hivyo kuchangia kujenga jamii yenye afya bora.

Sauti ya Juma Selemani Punda
Watoa huduma wa afya ngazi ya jamii wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mafunzo