Radio Jamii Kilosa

Chanjo hazipunguzi nguvu za kiume

28 August 2026, 13:43

Mratibu wa Chanjo wilaya ya Kilosa Lakia Ngayungwa akiwa katika kipindi maalumu Redio Jamii Kilosa. Picha na Amos Msingi

Jamii inahimizwa kupata taarifa sahihi kutoka kwa wataalamu wa afya na kuepuka imani potofu zinazoweza kuwafanya watu kukataa huduma za chanjo.

Na Asha Madohola

Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Kilosa, Lakia Ngayungwa, amewataka wananchi kuacha imani potofu kuhusu chanjo na kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo kwa wakati ili kuwalinda dhidi ya magonjwa mbalimbali hatari. Ngayungwa amesema chanjo ni muhimu katika kuzuia magonjwa ikiwemo kuharisha, kupooza, surua pamoja na saratani ya mlango wa kizazi kwa mabinti.

Akizungumza na Radio Jamii Kilosa, Ngayungwa amesema tangu kuanzishwa kwa huduma za chanjo, kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wilayani humo na kwamba hali ya sasa ni tofauti na ilivyokuwa hapo awali, ambapo Wilaya hiyo ilikuwa ikipoteza zaidi ya watoto elfu moja kwa mwaka, huku kwa sasa idadi hiyo ikiwa imepungua kwa kiwango kikubwa na kufikia chini ya watoto mia moja kwa mwaka.

Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Kilosa Lakia Ngayungwa

Aidha, Ngayungwa amekanusha taarifa na imani zinazodai kuwa chanjo husababisha wanawake kutopata ujauzito au kupunguza nguvu za kiume, akisema madai hayo hayana ukweli huku akieleza kuwa yeye mwenyewe alipata chanjo ya Corona pamoja na mumewe, lakini bado wameweza kupata mtoto, akitumia mfano huo kuonyesha kuwa chanjo haihusiani na changamoto hizo na pia amesema mabinti waliopatiwa chanjo ya HPV tangu mwaka 2018 wameendelea kukua na baadhi yao wamefikia hatua ya kupata watoto.

Hata hivyo, Ngayungwa amesema Serikali inaendelea kutumia fedha nyingi kuhakikisha chanjo zinapatikana na kutolewa kwa wananchi, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kuwapeleka watoto kupata chanjo bila kusubiri hadi wanapougua na amewataka wazazi wenye mabinti kuanzia umri wa miaka tisa kujitokeza na kuwapeleka kupata chanjo ya HPV, ambayo inalenga kuwakinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, huku akisisitiza kuwa jamii inapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwa wataalamu wa afya badala ya kuamini taarifa zisizo na msingi.

Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Kilosa Lakia Ngayungwa akizungumza