Radio Jamii Kilosa

Malezi bora kwa watoto wa Day Care

20 May 2026, 15:02

Wamiliki na walezi wa vituo vya kulelea watoto wadogo (Day Care) katika Kata ya Dumila wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa ustawi wa jamii. Picha na Aloycia Mhina

Watoto wa Day Care wanahitaji malezi bora, mazingira salama na elimu ya awali ili kuwajengea msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye.

Na Aloycia Mhina

Wamiliki na walezi wa vituo vya kulelea watoto wadogo (Day Care) katika Kata ya Dumila wilayani Kilosa wametakiwa kubadilika katika namna ya utoaji wa malezi kwa watoto ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia ya sasa yanayohitaji malezi bora na yenye kuzingatia maendeleo ya mtoto.

Katikati ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Silivesta Katikaza

Wito huo ulitolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Silivesta Katikaza wakati akifungua mafunzo ya siku 15 kwa wamiliki na walezi wa vituo 20 vya kulelea watoto wadogo katika Kata ya Dumila.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Katikaza alisema vituo vya kulelea watoto vina nafasi kubwa katika malezi ya awali na maendeleo ya mtoto, hivyo ni muhimu kwa wamiliki na walezi kuendana na mabadiliko ya sera na sheria za mtoto.

Aidha alisema kuwa hata sera ya mtoto ya mwaka 2008 ilifanyiwa maboresho na kupelekea kutungwa kwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo baadaye nayo iliboreshwa, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuendelea kujifunza na kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati.

Sauti ya Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Silivesta Katikaza akizungumza
Mratibu wa Mradi wa Kinara, Prisca Norbert

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kinara, Prisca Norbert alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapa elimu wamiliki na walezi wa vituo vya Day Care kuhusu usajili wa vituo vyao pamoja na mbinu za kujikwamua kiuchumi kupitia miradi na vikoba.

Sauti ya Mratibu wa Mradi wa Kinara, Prisca Norbert akizungumza

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Monika Gidioni na Saferini Makilila waliwashukuru waandaaji wa mafunzo hayo wakisema yatawasaidia kuboresha malezi ya watoto na kuinua hali zao kiuchumi.

Sauti za wamiliki wa vituo vya Day Care wakizungumza

Mafunzo hayo yanadhaminiwa na Taasisi ya Kinara kupitia mdau wa Swisscontact kutoka Morogoro kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu malezi ya watoto, usajili wa vituo pamoja na shughuli za maendeleo zitakazowaongezea kipato.