Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
20 May 2026, 14:08

Katika kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, kaulimbiu ya utunzaji wa mazingira 05 Juni 2026 inaendelea kuwa wito muhimu wa kujenga taifa lenye mazingira bora na maisha endelevu.
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kulinda mazingira na kuokoa vyanzo vya maji vinavyokabiliwa na changamoto za uharibifu pamoja na mafuriko.
Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa maeneo yanayoathiriwa na changamoto hiyo kupitia Mto Mkondoa ambao mara kwa mara husababisha mafuriko na athari kwa wananchi pamoja na shughuli za kiuchumi.

Katika hatua ya kuunusuru mto huo, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Mazingira, Baraka Haran Luvanda pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad Yusuf Masauni walifika katika eneo la Mto Mkondoa kwa ajili ya kukagua hali ya mazingira na kuzindua rasmi zoezi la upandaji miti kandokando ya mto huo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa alieleza kuwa juhudi za uhifadhi wa mazingira zinahitaji ushirikiano wa wananchi wote kwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa, ukataji miti holela unadhibitiwa pamoja na kuendelea kuhamasisha upandaji miti ili kupunguza athari za mafuriko zinazojitokeza kila mwaka.

Naye Msimamizi wa Maji kutoka Bonde la Wami Ruvu, Christian Kipyonda alisema uhifadhi wa Mto Mkondoa ni muhimu kwa ustawi wa mazingira na maisha ya wananchi, huku akisisitiza kuwa upandaji miti na utunzaji wa maeneo ya vyanzo vya maji ni sehemu muhimu ya kudhibiti mmomonyoko wa ardhi na kulinda rasilimali maji kwa kizazi cha sasa na kijacho.
