Radio Jamii Kilosa

DC Kilosa azindua Bima ya Afya kwa Wote

3 March 2026, 13:21

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka akizungumza wakati wa uzinduzi wa utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote kata ya Dumila. Picha na Elizabeth Makemba

Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni mpango wa Serikali ya Tanzania unaolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya bila kuathiriwa na gharama kubwa za matibabu na mpango huu unasimamiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Na Asha Madohola

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa amezindua rasmi mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kiwilaya katika hafla iliyofanyika Kata ya Dumila, akieleza kuwa utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya bila kikwazo cha kifedha.

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na serikali, awamu ya kwanza ya Bima ya Afya kwa Wote inalenga makundi maalum yakiwemo wazee, watoto, wajawazito pamoja na wananchi wenye kipato cha chini likiwa na lengo kuu la kupunguza gharama za matibabu kwa makundi hayo na kuwapatia uhakika wa kupata huduma bora za afya katika vituo vilivyosajiliwa bila kuchelewa au kunyimwa huduma kutokana na ukosefu wa fedha.

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka akikabidhi Bima ya Afya kwa mkazi wa Dumila

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa amesema kuwa zaidi ya wakazi elfu kumi wenye kipato cha chini wilayani humo wanatarajiwa kunufaika na mpango huo katika hatua ya mwanzo. Alibainisha kuwa tayari baadhi ya wanufaika wamekabidhiwa kadi zao za bima ya afya, huku zoezi la usajili kwa wananchi wengine wenye sifa likiendelea katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ili kuhakikisha hakuna anayesahaulika.

Sauti ya Mkuu wa wilaya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka akizungumza

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Morogoro wa National Health Insurance Fund, Mbala Shitindi, amesema kuwa jumla ya wananchi 10,615 wilayani Kilosa wanatarajiwa kunufaika na awamu hii ya kwanza na kwamba bima ya afya ina manufaa makubwa kwa wananchi kwani inawawezesha kupata huduma katika hospitali zote zilizosajiliwa nchini bila kubeba mzigo wa malipo ya papo kwa papo wanapougua.

Dkt Selemani Kasugulu Mkuu wa Divisheni ya afya, ustawi wa jamii na lishe

Naye Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Selemani Kasugulu amesema kuwa lengo la utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya kwa wakati, bila kikwazo cha gharama anapougua au anapohitaji matibabu huku akitoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga na bima hiyo.

Sauti ya Dkt Selemani Kasugulu Mkuu wa Divisheni ya afya, ustawi wa jamii na lishe akizungumza

Naye Afisa kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Silvery Maganza, amewahimiza wananchi wenye kipato cha chini kuitumia vyema fursa hiyo adhimu kwa kuwa gharama zote za bima hizo tayari zimelipwa na Mhe Rais na kueleza kuwa bima hiyo inabeba magonjwa mengi zaidi ya mia tatu na inamwezesha mwananchi kupata matibabu ya uhakika katika ngazi mbalimbali za huduma za afya.

Sauti ya Afisa kutoka Ofisi ya Rais Silvery Maganza akizungumza

Uzinduzi huo umeibua matumaini mapya kwa wakazi wa Dumila na maeneo jirani, ambao wamejitokea kwa wingi na kuahaidi kutumia siku hizo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kabla ya kukamilika kwa zoezi la usajili akiwemo Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Kefasi Joseph Kisiu ambaye ni mnufaika.

Sauti ya mkazi wa Dumila Kefasi Kisiu akizungumza
wanufaika wa mpango wa bima ya afya kwa wote wilayani Kilosa