Radio Jamii Kilosa

Kilosa kuadhimisha siku ya mazingira

4 June 2026, 15:34

Mhifadhi kutoka Idara ya Maliasili na Utunzaji wa Mazingira akiwa katika studio za Redio Jamii Kilosa akizungumzia maadhimisho ya siku ya mazingira wilayani Kilosa. Picha na Beatrice Majaliwa

Kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika upandaji miti, utunzaji wa vyanzo vya maji na matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira ili kujenga Tanzania ya kijani na salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Na Asha Madohola

Wananchi wa Wilaya ya Kilosa wametakiwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ili kufanikisha azma ya kuwa na Tanzania ya kijani ifikapo mwaka 2050, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofikia kilele chake Juni 5 mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Mhifadhi kutoka Idara ya Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Wilaya ya Kilosa, Haji Said, alipokuwa akizungumza na Redio Jamii Kilosa kwa lengo la kuitangaza kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani ya mwaka 2026 isemayo, “Dira ya 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.” ambapoamesema kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za vitendo katika kulinda na kuhifadhi mazingira kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla.

Wahifadhi kutoka Idara ya Maliasili na Utunzaji wa Mazingira wakiwa katika studio za Redio Jamii Kilosa

Amefafanua kuwa kukijanisha Tanzania kunamaanisha kulinda misitu, kupanda na kutunza miti, kuhifadhi vyanzo vya maji, kupunguza uchafuzi wa mazingira pamoja na kuhakikisha rasilimali za asili zinatumika kwa njia endelevu. Amesisitiza kuwa mafanikio ya Dira ya 2050 hayatapatikana kwa juhudi za serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi bila kujali umri au nafasi yake katika jamii.

Kwa mujibu wa Haji Issa, maadhimisho ya mwaka huu yanatoa nafasi kwa wananchi kutafakari mchango wao katika utunzaji wa mazingira na kuacha vitendo vinavyochangia uharibifu wa mazingira kama ukataji miti hovyo, uchomaji moto misituni na uchafuzi wa vyanzo vya maji na kila mti unaopandwa na kutunzwa leo ni hatua muhimu kuelekea Tanzania yenye mazingira bora na salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Sauti ya Mhifadhi Haji Said akizungumza

Aidha, amewahimiza wananchi wa Kilosa kujitokeza kwa wingi katika kilele cha maadhimisho hayo kitakachofanyika katika Shule ya Sekondari Chanzuru, Kata ya Chanzuru, ambapo shughuli mbalimbali za kimazingira zitafanyika ikiwemo upandaji miti na utoaji wa elimu ya uhifadhi. Amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kujifunza na kuimarisha mshikamano katika kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Sauti ya Mhifadhi Haji Said akizungumza