Radio Jamii Kilosa

UNICEF na Serikali yaimarisha malezi ya mtoto

10 May 2026, 11:52

Waandishi wa habari za watoto wakiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu jijini Dar es salaam. Picha na Elia Yunga

Familia bora ni msingi wa taifa imara kwani hujenga watoto wenye maadili, nidhamu na upendo ambao baadaye huwa wananchi wenye mchango katika maendeleo ya jamii hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuzingatia malezi yenye usawa na mawasiliano mazuri ili kuimarisha ustawi wa familia.

Na Asha Madohola

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuzingatia malezi yenye usawa wa kijinsia na kuepuka ukatili dhidi ya watoto ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye upendo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Malezi na Familia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Carlos Gwamagobe

Akizungumza katika mafunzo maalum ya waandishi wa habari za watoto kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Malezi na Familia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Carlos Gwamagobe alisema kuwa serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yanayozingatia upendo, ulinzi, maadili na usawa wa kijinsia kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Gwamagobe alieleza kuwa mafunzo hayo pia yanalenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa wazazi kuwa karibu na watoto wao, kusikiliza changamoto zao na kuwalea katika mazingira salama yasiyo na ukatili na kwamba ushirikiano kati ya serikali, vyombo vya habari na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhamasisha malezi bora yatakayosaidia kujenga familia imara na watoto wenye maadili mema.

Mratibu wa Programu ya Malezi na Familia kutoka wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu Victor Rugarabamu

Mratibu wa Programu ya Malezi na Familia kutoka wizara hiyo, Victor Rugarabamu alisema kuwa kupitia utafiti uliofanyika 2015 ilibainika kukosekana kwa malezi yanayozingatia usawa wa kijinsia katika familia ni miongoni mwa sababu zinazochangia kudorora kwa ustawi wa watoto nchini huku wito ukitolewa kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatoa malezi bora yenye upendo, usawa na ulinzi kwa watoto ili kuwajengea mazingira salama ya ukuaji na maendeleo.

Mwezeshaji Victor akizugumza
Mkufunzi wa Kitaifa Sabrina Majikata akitoa mafunzo kwa washiriki

Naye, Mkufunzi wa Malezi ngazi ya Taifa, Sabrina Majikata alisema kuwa mafunzo hayo yamejikita katika nguzo kuu tatu za malezi ambazo ni kumjali mtoto, kumlinda pamoja na kuzungumza naye kwa karibu pia tafiti zinaonyesha wazazi wengi wanakosa muda wa kukaa na watoto wao hali inayochangia kupungua kwa mawasiliano ndani ya familia.

Mkufunzi Sabrina Majikata akizungumza

Kwa upande wake Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabia za Jamii kutoka UNICEF, Alice Mwiru alisema kuwa shirika hilo linaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha ustawi wa watoto na kuimarisha malezi bora nchini.

Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia za jamii Alice Mwilo akizungumza

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Amina Semagogwa na Rugendo Madege walieleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kutoa taarifa sahihi kwa jamii kuhusu malezi na matunzo ya watoto pamoj na mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kuelimisha wazazi na walezi umuhimu wa kuwapa watoto malezi yenye upendo, ulinzi na usawa wa kijinsia.

Sauti za washiriki akiwemo Amina Semagogwe akizungumza
Wakufunzi na Washiriki ambao ni waandishi wa habari katika picha ya pamoja siku ya mwisho wa mafunzo kuhusu Familia Bora Taifa Imara