Radio Jamii Kilosa

Watumishi Kilosa wafanyiwa jambo

28 September 2026, 11:36

Pichani ni Watumishi divisheni ya utawala wakiwemo watendaji kata na vijiji waendesha ofisi pamoja na madereva wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa. Picha na Epiphanus Danford

Watumishi hao wameaswa kushirikiana pamoja katika masuala ya kiofisi.

Na Epiphanus Danford

Watumishi wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, wakiwemo Watendaji wa Kata na Vijiji, Waendesha Ofisi pamoja na Madereva, wamefanya ziara ya kutembelea Mbuga ya Wanyama Mikumi kwa lengo la kujenga mshikamano, kubadilishana uzoefu na kupata muda wa kupumzika pamoja baada ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya kila siku.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bwana Betuely Ruhega amesema kuwa ziara hiyo imelenga kuwaweka pamoja watumishi hao ili waweze kujenga mahusiano mazuri ya kikazi na kijamii, pamoja na kupata fursa ya kuondokana kwa muda na changamoto na majukumu mazito wanayokutana nayo katika utendaji wao wa kila siku.

Amesema kuwa watumishi hao wana nafasi kubwa katika kuhakikisha shughuli za Halmashauri zinaendelea kwa ufanisi, hivyo ni muhimu kuwapatia fursa ya kukaa pamoja, kuzungumza, kubadilishana mawazo na kujenga mshikamano miongoni mwao.

Sauti ya Mkuu wa divisheni ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa Betuely Ruhega

Aidha, Mkuu huyo ametoa wito kwa watumishi wanaopenda kuhamia na kufanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wanakaribishwa, akieleza kuwa Halmashauri hiyo ina mazingira mazuri ya watumishi kufanya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Sauti ya Mkuu wa divisheni ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa Betuely Ruhega

Kwa upande wake, Afisa Utawala, Sarah Chambo, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa watumishi kwa kuwa imewapa nafasi ya kukaa pamoja nje ya mazingira ya kawaida ya kazi na kushirikishana mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wao.

Sauti ya Afisa utawala Bi. Sarah Chambo

Sarah amesema kuwa kupitia ziara hiyo, watumishi wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wameweza kuzungumza kwa uhuru, kushirikishana uzoefu na kujenga uhusiano mzuri zaidi baina yao.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Mikumi Robert Charles ambaye ni mwenyeji wa eneo hilo, amesema amefurahishwa na uamuzi wa watendaji wenzake kutoka maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kutembelea Mbuga ya Wanyama Mikumi na kupata fursa ya kukaa pamoja.https://www.mikuminationalpark.net/

Sauti ya Mtendaji kata ya Mikumi Robert Charles

Amesema ziara hiyo imekuwa ya muhimu kwa kuwa imewapa watendaji hao nafasi ya kuzungumza, kubadilishana uzoefu na kufurahia mazingira ya Mbuga ya Wanyama Mikumi, jambo ambalo amesema linaweza kusaidia kuongeza morali na mshikamano katika utendaji wa kazi.

Ameongeza kuwa ziara kama hizo zina umuhimu katika kuimarisha mahusiano ya kikazi kwa watumishi, kwani zinawapa nafasi ya kukutana katika mazingira tofauti na yale ya kawaida ya ofisini na kujenga urafiki na mshikamano zaidi.

Ziara hiyo imehusisha watumishi kutoka kada mbalimbali chini ya Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, wakiwemo Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Waendesha Ofisi pamoja Madereva na wadau mbalimbali ambao kwa pamoja wanaendelea kuwa sehemu muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.