Hatimaye shule yanukia Serengeti Kyela
3 February 2024, 16:47
Baada ya kukosekana kwa shule za msingi na sekondari hatimaye wakaazi wa kata ya Serengeti hapa wilayani Kyela wanatarajia kuanza ujenzi wa shule baada ya kupatikana eneo.
Na Masoud Maulid
Kutokana na kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa kata ya serengeti wilaya ya kyela juu ya upatikanaji wa eneo kwa ajili ya kujenga shule ya msingi hatimae kilio hicho kimepata ufumbuzi.
Kata ya Serengeti ni Miongoni mwa kata zilizopo ndani ya mamlaka ya mji mdogo wa kyela toka kupatikana kwake haina shule ya msingi wala shule ya sekondari hali iliyosababishwa na ukosefu wa maeneo yaliyowazi kwa ajili ya kujenga shule hivyo wanafunzi kuwarazimu kutembea umbali mrefu kwenda kata zingine kwa ajili ya kupata elimu ya msingi na sekondari.
Akizungumza na Mwandishi wa Habari Afisa Mtendaji wa kata ya Serengeti Bonfance Kajuni amesema ili kupata eneo imewalazimu kuunda kamati kutoka kwenye vitongoji vitatu ndani ya kata hiyo,kwa lengo la kuendelea kutafuta eneo la kujenga shule,ambapo kamati imefanikiwa kupata eneo la kununua lenye thamani ni ya shilingi milioni hamsini.
Kajuni ameongeza kuwa baada ya kupata eneo hilo kamati imelazimika kwenda kwa wananchi kwa ajili ya kuwajulisha juu ya upatikaji wa eneo hilo,ambapo kila kitongoji kimeafiki na kukubali kuchangia kiasi kilichopendekezwa kwa awamu mbili ili kuhakikisha eneo hilo linakuwa mali ya kata ya serengeti.
Katika hatau nyingine Mtendaji huyo amewatoa hofu wananchi juu udhibiti wa michango itakayokusanywa kufanya kazi iliyokusudiwa,ambapo amebainisha kuwa wameandaa utaratibu wa kutoa risiti kwa kila mwananchi anayotoa fedha ya mchango na fedha zote zitatunzwa bank kupitia akaunti ya kata.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata ambaye pia ni diwani wa kata hiyo Martini Mwainyekule,amewapongeza wananchi kwa kukubali kwa kuchangia kiasi hicho kilichopangwa huku akisema kata ya Serengeti imekuwa na uhitaji mkubwa wa kujengwa kwa shule kutokana na shule ya msingi jirani ya Uhuru na Mbugani kuwa na wanafunzi wengi,hivyo kukamilika kwa ujenzi kutaondoa adhaa kwa wanafunzi na wazazi.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa kata ya serengeti Sakina minga, ameupongeza uongozi wa kata kwa kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa eneo hilo,ambapo ameongeza kuwa ni kilio cha muda mrefu hivyo ametoa wito kwa wananchi kila mmoja kujitoa kwa moyo ili kuanza kulipa kidogokidogo ili kuing`arisha kata ya serengeti kama zilivyo kata zingine.
Kata ya Serengeti ni mwiongoni mwa kata Mpya zilizozaliwa kutoka Kata ya kyela,ambapo zimepatikana kata ya serengeti,Mikoroshoni,Nkuyu, Ipyana,Bondeni,Mwanganyanga,Mbugani na Kata ya Itunge.