Mwanafunzi wa darasa tatu atumbukia mto Kiwira, hofu yatanda
15 May 2024, 18:48
Kutokana na kuharibika kwa kivuko cha Kasumulu kinachowaunganisha wananchi wa kata ya Ngana na Ibanda hapa wilayani Kyela kuwa katika hali mbaya wananchi wa kata hizo wameiomba serikali kuboresha haraka kivuko hicho kinachotishia uhai wao.
Na Masoud Maulid
Mtoto Elisha Godfrey Mwambwagilo mwenye umri wa miaka nane anahofiwa kufa maji baada ya kutumbukia mto kiwira akitokea kasumulu shule ya msingi kwenye kivuko cha mto kiwira.
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa kitongoji cha sama A John Mwaipopo anapoishi mtoto huyo amesema tukio hilo limetokea jumatatu may 13 2024 wakati mtoto huyo akitoka shule ya msingi kasumulu kurudi nyumbani ambapo baada ya kufika kwenye kivuko hicho cha kityeputyepu ambacho baadhi ya mbao zake zimeaharibika vibaya hali iliyopelekea mtoto huyo kutumbukia majini na kusombwa na maji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha kasumulu Nelson Minga ilipo shule ya msingi Kasumulu anaposoma mtoto huyo amesema, baada ya wananchi kupata taarifa ya kutumbukia motto kutumbukia mtoni wameshirikiana wananchi wote wa pande mbili kasumulu na Ibanda kuanza kumtafuta tangu siku ya tukio hadi siku ya tatu bila mafanikio.
Wakisimulia tukio hilo baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo wamesema wamesikitishwa na tukio la mtoto huyo anayehofiwa kufa maji huku wakiomba Serikali kuimarisha kivuko hicho kwa kuweka waya chini ili kusaidia pale mbao zinapoharibika au kujenga daraja la kudumu ili kuepusha maafa kama hayo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya kyela Josephine Manase ametoa pole kwa wazazi pamoja na wananchi juu ya tukio hilo, huku akiwataka kuendelea kushirikiana kumtafuta mtoto huyo na kuongeza kuwa serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini tarura watafanya kila linalowezekana kurekebisha kivuko hicho.
Aidha mkuu wa wilaya amewataka wananchi wote kuwa wasimamizi wa miradi inayokuwa inatekelezwa na serikali katika maeneo yao hususani kivuko hicho ambacho kimekuwa kikitumiwa vibaya kwa kupitisha mizigo mikubwa ambayo imekuwa ikileata uharibifu katika maeneo yao.
Mtoto Elisha Godfrey Mwambwagilo ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi kasumulu iliyopo kata ya ngana huku akisoma shule hiyo akitokea kata ya ibanda katika kiongoji cha sama A.