Keifo FM

21180 wapatiwa chanjo saratani mlango wa kizazi Kyela

8 May 2024, 17:29

Pichani ni mratibu wa chanjo wilaya ya Kyela Rosemary Tesha akizungumzia kuhusu utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi Picha na Nsangatii Mwakipesile

Wakati wa serikali na wadau mbalimbali wa afya kitaifa na kimataifa wakiendelea na juhudi za kutokomeza ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi jumla ya wasichana elfu ishirini na moja mia moja themanini wamepatiwa chanjo ya ugonjwa huo hapa wilayani kyela.

Na Zawadi Mwakijolo

Kampeni ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa watoto wa kike hapa wilayani kyela imekamilika huku watoto elfu ishirini na moja mia moja themanini wakifikiwa na wataalamu kutoka hospitali ya wilaya ya Kyela.

Kampeni hiyo imefanyika huku tathmini ikionesha kuwa watoto wa kike walio na umri wa kati ya miaka tisa hadi kumi na tano kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na matatizo ya saratani hali iliyolazimu serikali kutoa chanjo pamoja na elimu ya jinsi ya kujikinga na maambukizi yanayoweza kusabisha maradhi ya saratani.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kutoa chanjo hiyo katika maeneo mbalimbali hapa wilayani kyela mratibu wa chanjo Rosmery Tesha ameitaka jamii ya wanakyela kuona umuhimu wa watoto wao wa kike walio na umri huo kuwaruhusu ili wapate chanjo kwa ustawi wa afya yao ya uzazi kwa baadaye.

Sauti ya mratibu wa chanjo wilaya ya  Kyela Rosemary Tesha kuhusu jamii kuona umuhimu wa watoto wa kike kupata chanjo hiyo

Amesema kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni miongoni mwa magonjwa makubwa yanayosababisha vifo vya wanawake hapa Tanzania kutokana na wanawake wengi kukosa elimu ya ugonjwa huo na namna ya kujikinga na tatizo hilo.

Sauti ya mratibu kuhusu ugonjwa na hatari yake kwa wanawake hapa nchini

kuhusu idadi ya watoto wa kike waliopatiwa chanjo na elimu ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi amesema jumla yao ni elfu ishilini na moja mia moja na themanini licha ya changamoto ya mvua iliyosababisha mafuriko kukwamisha kufika baadhi ya maeneo yaliyopangwa kufikiwa na timu ya watalaam.

Sauti ya mratibu wa chanjo rosemary tesha kuhusu waliopatiwa chanjo

Ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi hapa nchini Tanzania umekuwa miongoni mwa magonjwa yanayowasumbua kina mama wengi hadi kusababisha vifo katika nyakati fulani hali inayoilazimu serikali na wadau mbalimbali kushiriki pamoja kumaliza tatizo hilo.