Askofu Rweyongeza aongoza maelfu ya Mahujaji Karagwe
15 September 2023, 12:22 pm
Kila tarehe 14 septemba waumini wa Kanisa katholiki jimbo la Kayanga wanakutana katika kituo cha hija Kalvario Kayungu kwa lengo la kusali njia ya msalaba ili kukumbuka mateso ya yesu aliyoyapata msalabani ili kuwakomboa wanadamu.
Na Eliud Henry
Askofu wa jimbo katoliki la Kayanga Almachiusi Vicent Rweyongeza amewaongoza Maelfu ya mahujaji katika misa ya msalaba katika kituo cha hija Kalivario Kayungu akiwataka kusameheana na kuwapenda maadui zao kwani kusamehe ni kutakasa kumbukumbu.
Hija hiyo imefanyika Septemba 14, 2023 ambapo Askofu ameanza kwa kubariki vituo vipya 15 vya njia ya msalaba vilivyojengwa upya katika mlima wa Kalvario uliopo katika parokia ya kimkakati ya Kayungu.
Akiongoza Misa Katika hija ya 13 kijimbo kijimbo Askofu Rweyongeza amesema lengo la hija na ziara ya msalaba ni kuimarisha imani ,upendo,ufuasi ,ushuhuda na mshikamano na Yesu pamoja kutubu na kumuomba Yesu wa msalaba.
Katika misa hiyo Askofu Rweyongeza amesema kuwa Yesu kristo akiwa msalabani kati ya maneno aliyosisitiza ni pamoja na msamah akimsihi Mungu kuwasamehe hata walio msurubisha ,hivyo wahumini hawana budi kusamehe ili kutakasa kumbukumbu ya mambo yaliyopita.
Amesema kuwa kuna makundi matatu ya kusamehe ikiwemo kujisamehe mwenyewe,kumsamehe mwenzako na kumsamehe Mungu akieleza kwa undani kuwa kujisamehe mwenyewe ni kuisamehe nasfi yako kutokana na mambo mabayo unayoitendea nafsi kwa uzembe.
Mkurugenzi wa hija jimbo katoriki la Kayanga Padre Nicolaus Byakatonda amesema kuwa kuna faida nyingi katika vituo hivyo na kuongeza kuwa kuna shuhuda nyingi za watu ambapo wengi wanaoenda kwa imani na kusali katika kituo hicho wengi wamepona magonjwa, pamoja kutatuliwa shida zao kutokana na imani ya kwa msalaba.
Nae Katibu wa Askofu padre Castor Tindyebwa akisoma salaam za askofu wa jimbo hilo amewasihi waumini na watu wote kutumia vituo hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kusali na kuomba na akawasihi kuacha matumizi mabaya ya vituo hivyo
Laurent Lauliani ni katekista katika Parokia ya Bushangaro kwa Upande wake amesema kuwa wakristo wanapokutana kwa pamoja katika Hija wanapa nafasi ya kusali pamoja na kupata Baraka kutokana na kutafakari matendo mema ya Mungu.