Karagwe FM
Karagwe FM
28 July 2025, 12:15 pm

Waganga wa tiba asili mkoani Kagera wamepewa angalizo dhidi ya wagombea wa udiwani na ubunge wanaotafuta ushindi kwa kutumia viungo vya wenye ualbino na ushirikina mwingine
Theophilida Felician.
Katibu mkuu wa chama cha waganga TAMESOT Bw Lukas Joseph Mlipu ametoa wito kwa waganga wa tiba asili nchini kufanya kazi kwa umakini hususani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2025.
Katibu huyo ameyabainisha hayo wakati akiwahutubia waganga kwenye semina iliyofanyika kata ya Kibeta manispaa ya Bukoba mkoani Kagera akifafanua kuwa imezoeleka nyakati kama hizi waganga huwa kimbilio la wanasiasa kupata tiba kwa namna mbalimbali hivyo ni wajibu wao kuwa chonjo kwani yamekuwepo mambo mengi yanayotendeka kwenye jamii yakiwemo mauaji ya watu wenye ualbino.

Mkuu wa polisi jamii mkoa wa Kagera ACP Mponder Rashidi kwa niaba ya kamanda wa polisi mkoani hapa amewaeleza kwamba baadhi ya waganga wa tiba asili wamekuwa wakihusishwa na ramuli chonganishi na kufanya kazi bila leseni mambo ambayo ni kinyume na taratibu
Mponder ameongeza kuwa kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais TAMESOT haina budi kuwasimamia kikamilifu waganga wasihusishwe na matukio ya namna yoyote kinyume na leseni zao.

Yustas Nyakubaho ni mwenyekiti wa waganga wa tiba asili wilaya Ngara akishukuru na kupongeza juhudi za katibu Mkuu Lukas Joseph Mlipu amewakumbushia madhira waliyoyapitia kipindi cha wimbi la mauaji ya Albino hivyo ametoa wito akiwasihi wenzake wasiingizwe mitegoni na watu wasiokuwa na nia njema na taaluma hiyo.
