Karagwe FM
Karagwe FM
6 July 2025, 5:58 pm

Kila zinapowadia nyakati za uchaguzi mkuu hapa nchini kunakuwa na ongezeko la matukio ya uhalifu yanayohusishwa na imani za kishirikina ikidaiwa kuwa ni kutekeleza maelekezo ya waganga wa tiba asili maarufu kama waganga wa kienyeji
Na Theophilida Felician, Bukoba
Chama cha waganga wa tiba asili TAMESOT nchini kimetoa wito kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaojishughulisha na kazi ya tiba asili bila kuwa na vibali vya kazi hiyo
Akizungumza hayo na chombo hiki kwa njia ya simu akiwa mkoani Dodoma katibu wa TAMESOT taifa Lukas Joseph Mlipu amesema kwamba changamoto ya watu kujipenyeza na kufanya kazi ya tiba asili imekuwa moja ya sababu ya kuchochea matukio ya ukatili hasa mauaji kwa jamii mara kadhaa.
“Mganga halali ni yule mwenye leseni kama hana leseni huyo siyo mganga bali ni tapeli, matapeli hawa wametuchonganisha na wananchi, imani yao kwetu inapungua, wanabakia na makovu ya maumivu makali pale yanapotokea matukio haya ya kikatili, jeshi la polisi linapowakamata watu hawa wakituhumiwa kuhusika na tukio wachunguze uhalali wa utambulisho wao maana mtu mwingine hata leseni hana lakini anatamba mtaani kuwa anatoa tiba asili matokeo yake yanashuhudiwa madhara kwa wananchi” amesema Mlipu.
Sambamba na hilo ameliomba baraza la tiba asili na tiba mbadala chini ya wizara ya afya kutoa usajili kwa mtu anayestahili iwapo anakidhi vigezo vya kuwa mganga itasaidia pia kuwabana wale wote walioigeuza tiba asili kama chaka la kujificha na kufanya uovu.
Katibu Lukas ameongeza kuwa zipo changamoto nyingi zinazoikabili tiba asili hususani kutokuwa na wawakilishi kwenye vyombo vya maamuzi likiwemo Bunge ambapo ameeleza wakiwa na mwakilishi huko Bungeni angalau kupitia nafasi 10 za viti maalumu zinazoteuliwa na Rais itasaidia kuchechemua sekta hiyo.
Hata hivyo ametoa onyo kwa waganga walio halali kamwe kutokujiingiza mtegoni na kushiriki ramli chonganishi huku akilaani tukio la watu wawili kukutwa na viungo vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu katika manispaa ya Bukoba tukio lililotolewa taarifa na kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Kagera Blasius Chatanda hivi karibuni.