Karagwe FM

SHIVYAWATA Bukoba walalamikia kukosa fursa za kiuchumi

19 May 2025, 1:34 pm

Baadhi ya wanachama wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA mkoa wa Kagera. Picha na Theophilida Felician

Licha ya kila halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu, Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA manispaa ya Bukoba mkoa wa Kagera wamelalamikia kutonufaika na asilimia mbili inayotengwa kwa kundi hilo wala kuingizwa katika mradi wa kaya masikini TASAF.

Theophilida Felician.

Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wamelalamikia changamoto ya kutokupewa kipaumbele cha nafasi ya kushiriki fursa mbalimbali hususani mikopo na kuingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF.

Wamezungumza hayo kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwao maeneo ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera manispaa ya Bukoba.

Petronida Mwijage na Anna Kajuna mwenye mtoto anayeishi na ulemavu wa akili wamefafanua kwamba wanakabiliwa na changamoto zinazowasababishia kuishi katika mazingira magumu kutokana na ukosefu wa mitaji ya kuwawezesha kuendesha shughuli za kuingiza kipato badala yake wamebakia kuwa ombaomba jambo ambalo wamelitaja kama fedheha.

Petronida Mwijage na Anna Kajuna
Wajumbe wa SHIVYAWATA wakiwa katika kikao. Picha na Theophilida Felician

Wajumbe hao akiwemo mwenyekiti Joseph Novati Mwijage, Katibu Vaileth Augustine, Anna Kajuna naye Petronida Mwijage wametoa kilio chao kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wakimuomba kulitizama kwa jicho la kipekee kundi la watu wenye ulemavu kupitia nyanja tofauti kwani hata vyama vyao uendeshwaji wake bado umekuwa shida kutokana na kutokuwa na ruzuku hivyo wamebakia kusota kwa kuchangia chochote ili waweze kuendesha vyama hivyo.

Hata hivyo wameishauri serikali kuona umuhimu wakuwaweka serikalini wawakilishi wa viongozi kuanzia ngazi ya chini hadi bungeni watakaoweza kuwasemea moja kwa moja changamoto zao kuliko hali ilivyo kwa sasa.