Karagwe FM

Wafanyabiashara Bunazi walalamikiwa kwa uchafuzi wa mazingira

5 February 2025, 9:41 pm

Eneo la kutupa taka (dampo) zinazozalishwa katika soko la Bunazi. Picha na Respicius John

Wananchi waishio kando ya masoko na magulio nchini wamekuwa wahanga wa harufu mbaya na pengine hofu ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na mlundikano wa taka kando ya makazi yao

Na Respicius John, Missenyi

Wananchi wanaopakana na soko la Bunazi wilayani Missenyi mkoani Kagera wamelalamikia uchafuzi wa mazingira unaohatarisha afya katika maeneo yao wanaodai kuwa unafanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaoshindwa kulipia huduma ya choo.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na soko la Bunazi wamesema kuwa kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira unaohatarisha afya zao na kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanajisaidia mashambani mwao kwa kushindwa kulipia gharama za vyoo

Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na soko la Bunazi
Baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Bunazi. Picha na Respicius John

Kwa upande wa wafanyabishara wanadai kuwa wanashindwa kumudu gharama za choo kila wanapobanwa na haja kutokana na kutumia muda mwingi sokoni hapo ambapo hata hivyo uongozi wa soko hilo umeiomba halmashauri ya wilaya kulegeza gharama za matumizi ya vyoo kwa wafanyabiashara wa kila siku

Sauti ya wafanyabiashara wa soko la Bunazi
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi Projestus Tegamaisho akiongea na wafanyabiashara wa soko la Bunazi. Picha na Respicius John

Baada ya kutembelea soko la Bunazi na kushuhudia uchafu katika dampo lililopo karibu na makazi ya watu pamoja na kupokea changamoto ya gharama za matumizi ya vyoo kwa wafanyabiashara, mwenyekiti wa halmashauri ya Missenyi Projestus Tegamaisho ameahidi kushughulikia kero hizo sambamba na kuwasiliana na mkurugenzi wa halamashauri ya Missenyi ili kuona namna ya kurekebisha gharama za matumizi ya vyoo vya soko la Bunazi

Sauti ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi Projestus Tegamaisho